Home » » Godoro, miti ilivyowaokoa watu kifo Dumila-2

Godoro, miti ilivyowaokoa watu kifo Dumila-2

Mmoja wa watu ambao wamepatwa na mkasa huo wa mafuriko anasema akiwa amelala usingizi alishangaa akivamiwa na maji.
Mwananchi huyo Shida Abdallah anasema baada ya kumtokea hali hiyo hakuwa na namna ya kujiokoa kwani hakuweza kuona sehemu ya kukimbilia na kulikuwa na giza.
Maji hayo yalimvamia na akajikuta anapelekwa yalikokuwa yakielekea kwani yalikuwa na kasi mno; anashukuru kwamba aliuona mti ambao aliushika kwa nguvu na kuupanda.
“Yale maji yalinistukiza na nilikuwa nimelala usingizi, baada ya kunisomba yalinipeleka umbali mrefu, yakanileta hadi kwenye mti; yakanileka katika mti wa kwanza yakanizungusha, nilipojaribu kuushika nikashindwa na kunipeleka mbele ambako kwa bahati nzuri pia kulikuwa na mti mwingine, yakanizungusha hapo, nashukuru nilifanikiwa kulishika tawi na kuling’ang’ania.
“Nilifanikiwa kuupanda mti huo na kukaa juu kwa zaidi ya saa 12 bila nguo, kwani nilivaa nguo ambazo ni za kulalali, zilitoka zote wakati wa hekaheka za kujiokoa,” anasema Abdallah.
Fadhil Masanzanzia (32) ndiye kijana aliyeongoza kujitosa katika maji ya mafuriko kupiga mbizi na mwenzake Hassan Rajab na Sud Alfan Sud kuongoza msafara wa waokoaji kumfuata Shida Abdallah kumwokoa, wanaeleza ugumu wa kazi hiyo.
Masanzanzia anasema kuwa haikuwa kazi rahisi kumfikia, walikumbwa na vikwazo vingi ndani ya maji hayo ikiwamo kujigonga mwilini na mawe, magogo na maji.
“Kikundi chetu kilikuwa na wapiga mbizi 18 lakini watu ambao tulikuwa mstari wa mbele na uwezo wa kuwafikia wahanga tulikuwa hatuzidi watano, tunashukuru tumefanikiwa kuwaokoa watu zaidi ya saba kutoka juu ya miti na kuwafikisha nchi kavu tukitumia madumu tupu ya ujazo wa lita 20”. anafafanua Masanzanzia.
Mwanzo ilionekana kazi ya kuwaokoa watu waliokwama katika miti ni ya kujitolea lakini tunamshukuru sana Naibu Waziri wa Ujenzi na kuthamani juhudi zao na kutoa fedha Sh40,000 akifuatiwa na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera aliyetoa Sh25,000 na kaka wa Hatibu Bakari, Makongoro Bakari kutoa kiasi cha Sh10,000 baada ya kumwokoa ndugu yake.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Magole kilichopo tarafa hiyo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Hussein Nyongo anasema sehemu kubwa ya waathirika wa mafuriko hayo ni wale wa mtaa wa Bwawani kutokana na eneo hilo kuwa ndiko yalikoanzia mafuriko kutokana na kuwa na kingo za tuta kwenye barabara iliyosababisha makaravati kuziba uchafu na maji kutuwama.
Kijiji hicho cha Magole kina mitaa sita lakini wananchi wake walioathirika zaidi ni wale wa mitaa ya Bwawani, Kichangani, Manyata na Zizini huku wale wa mitaa ya Magengeni na Mjimkuu wananchi wakiathirika kidogo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliiponda ripoti ya mafuriko ya tarafa ya Magole na kuwataka viongozi wa mkoa kuirudia upya ili kupata idadi kamili ya waathirika na kujua namna ya kuwasaidia.

Kikwete aliiponda ripoti hiyo baada ya kutoridhishwa na taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kwa niaba ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa taasisi akisema kuwa wananchi 12,472 wamepoteza makazi huku nyumba1,141 zikibomoka kutokana na mafuriko hayo na nyumba 2,759 zikiingiliwa na maji na kuhitajika kiasi cha sh53.7milioni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya muda.
Kikwete alikataa ripoti hiyo kutokuwa na ripoti hiyo kutokuwa na mchanganuo idadi ya waathirika.
“Nataka kujua idadi ya wananchi walioathirikana na mafuriko haya, idadi ya watu wapo wangapi kwa maana ya wanaume, wanawake, watoto na wazee, je, wale nyumba zao zimebomoka kwa sasa wamehifadhiwa wapi,” anahoji Kikwete.
Maswali hayo yalishindwa kupatiwa majibu na Mkurugenzi wa halmashauri ya Kilosa alipotaka kujibu, na kumfanya mkuu huyo wa nchi kucheka.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa