WAKULIMA wa zao la tumbaku nchini, wameahidi kuongeza juhudi za
kulifanya liwe bora zaidi ikiwa ni pamoja na kulitunza, kulichambua na
kuondoa uchafu kabla ya kuliuza, ili lifikie viwango vya ubora wa
kimataifa.
Hayo yalibainishwa jana na baadhi ya wakulima wa zao hilo kutoka
wilaya za Mlele na Mpanda mkoani Katavi, walipofanya ziara ya mafunzo
kwenye Kiwanda cha Kusindika Tumbaku Tanzania (TTPL) cha mjini Morogoro.
Wakulima hao wametoka kwenye vyama vitatu vya ushirika vya msingi
ambavyo ni Ilunde kilichocho Kata ya Inyonga wilayani Mlele na vyama
vya msingi vya Mishamo na Katumba vilivyopo wilayani Mpanda.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, walisema wameshuhudia uchafu wa
aina mbalimbali kama manyoya ya ndege, kokoto, vipande vya plastiki
ukiondolewa kwenye tumbaku kabla ya kusindikwa kiwandani.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Mishamo, Pilidas Anacredo, alisema
ziara hiyo imewafumbua macho hususani baada ya kugundua kazi ya
kuisindika tumbaku inakuwa ngumu zaidi kiwandani pale ambapo inapokuwa
imechanganywa na uchafu.
“Tusipoboresha zao hili, kwa kweli hatuwezi kulifikisha kwenye
viwango vya ubora vya kimataifa ambako ushindani ni mkubwa, hivyo
tunaporejea majumbani tutazidi kueneza ujumbe huu ili ufike mbali
zaidi,” alisema.
Akizungumzia mafanikio anayoyapata kwenye tumbaku, alisema zao hilo
analolima kwenye ekari 22 kila mwaka linamuingizia sh milioni 12,
ambazo zimemsaidia kujenga nyumba bora na ya kisasa, kusomesha watoto
kwenye shule nzuri na kumiliki magari.
Mkulima mwingine kutoka Chama cha Msingi Ilunde, Martin Mlonga
alisema ziara hiyo imewafundisha mambo mengi ikiwemo kufahamu zaidi
mfumo wa biashara ya tumbaku kuanzia usindikaji hadi uuzaji wake.
Maofisa wa TTPL waliwaasa wakulima hao kuliboresha zao hilo, kwani
faida zake zina manufaa kwa wakulima, wanunuzi na taifa kwa jumla.
Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya Tumbaku Tanzania Leaf
Tobacco Company Limited (TLTC) ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi wa
Kampuni ya Tanzania Tobacco Proceesors Limited (TTPL), Richard Sinamtwa
alisema zao hilo linanufaisha wakulima hao na taifa kwa ujumla, hivyo
ubora wake ni muhimu ili liweze kushindana kwenye soko la kimataifa.
“Kwa mfano kiwanda kinapokuwa kinafanya kazi zaidi ya watu 5000
hunufaika na ajira ya moja kwa moja hapa, TANESCO inalipwa zaidi ya
shilingi milioni 300 kwa mwezi, manispaa inalipwa kodi mbalimbali
ukiachia mbali serikali kuu inayolipwa kodi kutoka kwenye zao hili,”
alisema.
Meneja wa Kilimo na Shughuli wa TLTC, Louis Rousos alisema lengo la
ziara hiyo ni kuwaonyesha wakulima hao namna bora ya kulihudumia zao
hilo kuanzia mashambani hadi ghalani na kujionea vionjo vya wateja.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment