HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetenga kiwanja namba 675
kitalu ‘E’ chenye zaidi ya ekari 10 kilichoko kata ya Tungi kwa ajili
ya makaburi.
Utengaji wa kiwanja hicho umekuja baada ya eneo hilo kuvamiwa na matapeli kisha kuuza kinyemela.
Eneo hilo ambalo siku za karibuni limeamsha tafrani baada ya kujikuta
likijengwa bila utaratibu na watu wanaodaiwa kuuziwa viwanja na
matapeli, limemlazimu Mkurugenzi wa Manispaa Jorvis Simbeye kumwagiza
Ofisa Mtendaji Abuu Liwangila kata ya Tungi Liwangila kulilinda eneo
hilo kwa shughuli hizo.
Kwa mujibu wa barua ya Ofisa Mtendaji kwenda kwa Mkurugenzi wa
Manispaa, kiwanja hicho sasa kimepimwa kwa kuzingatia ramani ya mipango
miji namba10/178/996 na kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji na
Vijiji nchini kupitia Wizara ya Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi
3/3/1997.
“Pia ramani ya kiwanja hicho iliidhinishwa na mkurugenzi wa ramani
na upimaji Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
26/07/2006…ofisi inakujulisha na kukuthibitishia kuwa eneo namba 675
kitalu ‘E’ Tungi ni kwa ajili ya matumizi ya kuzikia na si vinginevyo,”
alifafanua Mtendaji kupitia barua hiyo.
Salumu Tonyoke mkazi wa Tungi alipongeza uamuzi huo wa manispaa
akisisitiza kuendelea kusimamia vema maeneo ya wazi na shughuli maalumu
kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Mbali na hilo aliitaka serikali kuhakikisha inapima maeneo mapema na
kuwagawia wananchi hata kwa mkopo ili kukomesha wimbi la makazi holela.
“Unajua watu wanalazimika kutapeliwa kiurahisi kutokana na mfumo
mbovu wa kimaslahi binafsi uliojaa serikalini, viwanja vinapimwa
vichache, vyote vinachukuliwa na madiwani na watendaji wa serikali ili
waje wawauzie wananchi kwa bei ya kuwalangua, sasa wananchi hawana
uwezo wa kununua bei zao wanaona ni bora wakanunue kwa mtu bila kujali
lolote,” alifafanua Tonyoke.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment