Watu
watatu wanadaiwa kufariki dunia akiwemo askari polisi na wengine watatu
kujeruhiwa kutokana mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wa jamii ya
Kisukuma katika Kijiji cha Igwati, Tarafa ya Malinyi wilayani Ulanga.
Taarifa
zilizopatikana kutoka eneo la tukio zimedai kuwa wakulima walivamia
kituo cha polisi kwa lengo la kushinikiza wenzao watatu kuachiwa baada
ya kukamatwa wakituhumiwa kumuua mfugaji aliyetambulika kwa jina la
Matanyi Luchoma (16). Ilidaiwa kuwa wananchi hao baada ya kupata
taarifa za kukamatwa kwa wenzao walifika kituo cha polisi ambapo,
hawakuwakuta watuhumiwa hao baada ya polisi kuwahamishia kituo kingine
na hivyo kuamua kuchoma moto kituo hicho pamoja na gari la askari. Wananchi
hao walifanya vurugu kituoni, ambapo yalitokea mapigano kati yao na
polisi, hivyo kumuua askari mmoja na askari nao kuwaua wananchi wawili
na kujeruhi wengine watatu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
alipotafutwa kuthibitisha tukio hilo, simu yake ilikuwa haipatikani.
Hata hivyo alipotafutwa Kaimu Kamanda wa Polisi, John Laswai, alikiri
kutokea tukio hilo na kwamba Kamanda alikuwa eneo la tukio. Mgogoro
huo unadaiwa kuanza Desemba 13, mwaka huu saa 2 usiku katika Kijiji cha
Igwati Malinyi wilayani Ulanga ambapo kundi la wananchi lilimkamata
mfugaji huyo mkazi wa Lupeleme na kumpeleka katika ofisi za kijiji cha
Lugawa. Ilidaiwa kuwa baada ya kumfikisha kwenye ofisi hizo,
mtendaji alimfungia mtuhumiwa ndani na kuanza kuhoji sababu ya wananchi
kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo halikuwapendeza, hivyo kuanza
kumshambulia mtendaji huyo hadi akakimbia. Alisema walivunja ofisi na kisha kuanza kumpiga kijana huyo hadi kusababisha kifo chake. Hata
hivyo ilidaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo kilisababishwa na baadhi ya
watu wanaodaiwa kuwa wafugaji wa jamii ya Kisukuma kuvamia nyumbani kwa
mjumbe wa kamati ya mazingira, Victoria Marietha, kisha kumpiga na
kumsababishia majeraha. Mjumbe huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugala, Tarafa ya Malinyi ambapo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment