WAKULIMA wa Wilaya ya Kiteto, Manyara, wameomba serikali iwape
kibali cha kuwaondoa wafugaji kama yenyewe serikali imeshindwa kutatua
mgogoro huo ambao umedumu kwa miaka mingi.
Wakulima walitoa kauli hiyo juzi muda mfupi baada ya kuvunjika kwa
mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wafugaji kwa ajili ya kupinga kauli
ya Naibu Spika na mbunge wa Kongwa Job Ndugai (CCM) aliyesema viongozi
wa Dodoma na Manyara wameshindwa kutatua mgogoro kati ya wakulima na
wafugaji kutokana na kuwepo kwa vitendo vya ukabila.
Mkulima Iddi Shabani alisema wakulima wamechoshwa na vitendo vya
unyanyasaji wanavyofanyiwa na wafugaji kwa kushirikiana na baadhi ya
viongozi wa serikali.
Shabani alisema kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa miaka mingi kati ya
jamii ya wakulima na wafugaji wakati taarifa zikiwa zinawafikia
viongozi wameshindwa kutatua mgogoro huo sasa umefika wakati wa kuomba
wapewe kibali cha kufanya vita kati ya wakulima na wafugaji.
“Mgogoro huu ni wa miaka mingi sasa tumekuwa tukiwaambia viongozi wa
Dodoma na Manyara lakini hakuna kinachofanyika na sasa tunamuomba
Waziri Mkuu afike eneo hili atusikilize… lakini kama hawezi basi
tunamuomba rais afike watusikilize,” alisema.
Alisema kitendo cha wakulima kuendelea kufukuzwa na kunyanyaswa na
kundi la wafugaji ni jambo linalosababishwa na ubaguzi wa kikabila
unaofanywa na watendaji ndani ya serikali kwa kuwapendelea wafugaji
ambao ni Wamasai na kuwanyanyasa wakulima.
“Tunashangazwa na serikali kuwapa kipaumbele wafugaji ambao kazi yao
kubwa ni kufuata mikia ya ngo’mbe huku hata hawana mahali pa kuishi kwa
maana ya kutokuwa na nyumba lakini wakulima wanaolisha nchi nzima
wanaendelea kunyanyaswa jambo ambalo halikubaliki,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment