Morogoro. Manispaa ya Morogoro ni moja ya
maeneo ambayo yameathiriwa na Ukimwi ambao kichocheo chake kikubwa ni
mwingiliano wa kibiashara yakiwamo magari makubwa kama malori ambayo
huegeshwa mjini humo likiwamo eneo maarufu la Itigi.
Eneo hili limekuwa maarufu kwa umalaya kwani
nyakati za usiku malori mengi huegeshwa katika maeneo hayo na kuwa
kishawishi kikubwa kwa baadhi ya watu wakiwamo vijana hasa wasichana
ambao wamekuwa wakishiriki biashara ya ngono.
Kinadada kutoka kila kona ya Morogoro hufika Itigi kwa kufanya biashara hiyo ya uchangudoa.
Miongoni mwao wamo wanafunzi kutoka vyuo
mbalimbali vilivyoko Morogoro ambao hujihusisha na ngono. Vijana hao
wasomi wa vyuo vikuu mbalimbali wamekuwa wakifanya vitendo hivi bila
kujali kuwa Ukimwi bado ni tishio.
Baadhi yao wanadai kuwa wanafanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.
Dk Getrude Lebby, mratibu wa Ukimwi Wilaya ya Morogoro Mjini anaeleza kuwa kinamama ndiyo wameambukizwa zaidi kuliko wanaume.
Dk Lebby anasema kuwa maambukizi ya Ukimwi wilayani humo yamekuwa yakisababishwa zaidi na:
Kwanza, vigodoro-harusi, ngoma za kunema wari ambazo zimekuwa zikichezwa hasa nyakati za usiku.
Pili, barabara kuu ya Iringa, Dodoma, Dar es
Salaam ambayo huwezesha madereva wengi wa malori hasa ya mizigo kuegesha
eneo la Msamvu.
Sababu nyingine ni wingi wa taasisi za elimu ya
juu kama vile, Kigurunyembe, Mzumbe, Sokoine, Jordan na Chuo Kikuu cha
Kiislamu ambazo wanafunzi wake wamekuwa wakishiriki ngono bila
tahadhari.
Pia, Morogoro kuwa Kitovu cha biashara zikiwamo za
mazao ya kilimo kama mchele kutoka Kilombero, Mahenge na Ifakara,
viwanda vya sukari Mtibwa na Kilombero.
Viwanda mbalimbali mjini humo vinavyohitaji nguvukazi . Hivyo ni pamoja na vya tumbaku, nguo na ngozi
Mtaalamu huyo anaeleza kitakwimu kuwa maambukizi ya VVU yamekuwa yakipanda na kushuka kila mwaka.
Amir Nondo Meya wa Morogoro anasema kuwa hana
taarifa yeyote kuhusu mazingira hatarishi kama ya Itigi na Kaumba bali
anachokijua kuwa maeneo hayo ni maarufu kwa kumbi za starehe.
“Ninachokijua mimi ni kuwa maeneo hayo ni maarufu kwa starehe watu
mbalimbali huenda maeneo hayo kwenda kuburudika na si vinginevyo”anasema
Nondo.
Hata hivyo, ngono zinazofanyika Itigi ni kama mapenzi ya kuku ambayo hufanyika popote.
Uchunguzi unaonyesha kuwa chumba kimoja kidogo
hutumiwa na watu zaidi ya sita kwa wakati mmoja na mmiliki wake kupata
Sh1,000 kwa kila mtu anayehudumiwa.
Takwimu za maambukizi ya VVU Morogoro zinaonyesha
kuwa jumla ya watu 12,482 waliopima VVU, wanaume 6,371 na wanawake
6,111, kati yao waliopatikana na maambukizi ni 668 wanaume 253 na
wanawake ni 415.
Enedy Mwanakatwe, Mratibu na mshauri wa Ukimwi
wilaya anasema kuwa ili kuhakikisha maambukizi ya VVU yanapungua ni
wajibu wa kila mtu kuchukua hatua kwa jamii pia elimu kuhusu Ukimwi
itolewe kwa wanafunzi.
“Moja ya mikakati ni kuanzisha Klabu za
afya/Ukimwi kwenye vyuo vikuu, vyuo vya kawaida na shule zetu ili tuweze
kupunguza maambukizi kwani Ukimwi upo na unaua,”anasema.
Mwanahawa Hamis na Happiness John na ni miongoni
mwa kinadada wanaojihusisha na biashara hiyo ya ngono ambao wanasema
kuwa hufanya biashara hiyo kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili.
“Maisha bwana kila mtu anajua anavyoishi kujikimu
kimaisha, wapo wanaoiba mali za watu, majambazi, mafisadi na malaya kama
sisi lakini hatufanyi hivyo kwa kupenda ni ugumu wa maisha ndiyo
unaosababisha japokuwa wapo wanafanya hivyo kwa tamaa zao kama wanafunzi
wa vyuo,” alisema Mwanahawa.
Happiness anasema kuwa ukosefu wa ajira nchini
ndiyo chanzo cha yote haya kwani kila mwaka wasomi kwa kila, idara
wanaongezeka, lakini hakuna ajira.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment