Home » » Hali sasa ni shwari Malinyi

Hali sasa ni shwari Malinyi

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Faustine Shilogile
 
Jeshi la Polisi kupitia timu maalumu kutoka makao makuu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni Mafunzo, Paul Chagonja limewasili katika mji wa Malinyi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi na kuawa kwa watu watatu na askari wa kituo hicho cha Malinyi wilayani Kilombero jana.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Faostine Shilogile, alisema kikosi hicho kwa kushirikiana na askari kutoka mkoani Morogoro waliwasili juzi jioni.

 Alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na vurugu hizo na kwamba hali ya usalama imeanza kuimarika katika kijiji hicho huku askari wakiendelea kuimarisha ulinzi.

Kwa mujibu wa Shilogile, taratibu za uchunguzi wa kidaktari wa miili ya marehemu ambao ni wakulima zimeshakamilika na tayari marehemu hao wameshazikwa.

Alisema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuchukua maelezo kutoka kwa watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo na  baada ya uchunguzi huo atatoa taarifa katika vyombo vinavyohusika.

Pia alisema kuwa baada ya uchunguzi huo kukamilika watuhumiwa wa mauaji hayo pamoja na watu waliohusika kuchochea na kuanzisha vurugu hizo watafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

“Tunafanya uchunguzi kwa kuwa moja ya  kazi ya polisi ni kujilinda mwenyewe hasa wakati yanapotokea machafuko ama vurugu hivyo uchunguzi unaofanywa utabaini mazingira ya tukio hilo na kujua uhalali wa nguvu waliyoitumia polisi katika tukio hilo hasa katika kujiahami wao wenyewe, kulinda silaha walizokuwa nazo, kuokoa kituo cha polisi kilichotaka kuchomwa moto pamoja na magari na pikipizi za polisi,” alisema Shilogile.

Tukio hilo la mauaji lilitokea juzi asubuhi baada ya wakazi wa kijiji cha Igawa Malinyi Ulanga kuandamana na kuvamia kituo cha polisi cha Malinyi kwa lengo la kuwatoa wenzao waliokamatwa kwa tuhuma za kumuua mfugaji wa jamii ya Kisukuma, Matanji Luhembe (16).

Mauaji ya mfugaji huyo yanadaiwa kutokana na kisasi kilicholipizwa na wakulima baada ya wafugaji wa jamii ya Kisukuma kumuua mjumbe wa kamati ya mazingira ya kijiji hicho Desemba 13, mwaka huu. 
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa