Home » » Mzumbe kushirikisha jamii ujenzi wa miundombinu

Mzumbe kushirikisha jamii ujenzi wa miundombinu


Chuo Kikuu Mzumbe
Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu, kinatarajia kuishirikisha jamii kushiriki kujenga miundombinu kwa makubaliano maalum ili kukidhi mahitaji halisi ya miundombinu ya kutolea elimu ya juu kwa Watanzania.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho Utawala na Fedha, Profesa Faustin Kamuzora, aliyasema hayo wakati wa mahafali ya 12 yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki.

Profesa Kamuzora alisema kuwa chuo hicho kimeweka mpango huo ili kukidhi mahitaji ya utoaji elimu ya juu nchini.

“Chuo chetu kwa sasa kimebadili sera na kinahitaji jamii ishiriki katika ujenzi wa miundombinu,” alisema.

Alisema Chuo kipo katika hatua za mwisho kumalizia mkakati wa kuiweka ardhi yake vizuri na baada ya kukamilika maeneo yatatengwa wenye fedha wafike kujenga miundombinu ya kitaaluma ikiwamo madarasa ya kufundishia, maktaba, ofisi za walimu na mabweni.

Pia alisema kwa upande wa Kampasi ya Dar es Salaam, wamejenga jengo la ghorofa tano na linatarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Desemba 21, mwaka huu.

Kwa upande wa Kampasi ya Mbeya, alisema jengo la maktaba limekamilika na sasa wanaendelea kuweka vifaa mbalimbali vya kimaabara kwa ajili ya masuala hayo ya kitaaluma.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Profesa Josephat Itika, alisema Chuo kinaendelea kufanya vizuri kitaaluma kutokana na walimu wanafanya kazi nzuri ya kufundisha.

“Kwa mfano, katika mahafali haya ya 12 Chuo kimetoa zawadi kwa walimu kwa michango yao mbalimbali kitaaluma,” alisema na kufafanua kuwa baadhi ya michango hiyo ni pamoja na kufanya tafiti na kuandika vitabu na makala zinazotumika kufundishia.

Aliongeza kuwa vitabu na makala hayo pia hutumika kutoa ushauri kwa serikali, wizara mbalimbali, mashirika ya serikali na sekta binafsi katika kusaidia masuala ya kiuchumi, siasa na kijamii.

Alisema vitabu hivyo na makala hujazia vitabu vile vilivyoandikwa kimataifa, hivyo kazi ya Chuo ni kuhamasisha na kuwatambua walimu kwa kazi nzuri ya kuendeleza elimu ya juu.

Alifafanua kwamba matokeo ya kazi nzuri ya utafiti na kuandika machapisho mbalimbali husaidia kila mwaka wahitimu kuwa bora zaidi kwa vile wanapata elimu inayoendana na mazingira yanayowazunguka.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa