Morogoro. Watu watatu wamefariki dunia katika
matukio tofauti yaliyotokea mkoani Morogoro likiwemo la mlinzi wa mnara
wa kampuni ya simu kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani
wakati akiwa lindoni.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Faustine Shilogile
alimtaja mlinzi aliyeuawa kuwa ni Hamisi Mtini (65) Mkazi wa Kihonda
Mbuyuni Manispaa ya Morogoro.
Alisema tukio hilo lilitokea Desemba 29 mwaka huu
saa 1:30 asubuhi eneo la Kihonda Mbuyuni ambapo mlinzi huyo aliuawa na
watu wasiojulikana kisha watu hao waliiba betri za mnara wa Kampuni ya
Simu ya Tigo.
Aidha Mwanne Omary (43) Mkazi wa Ipugusa Mlimba
Wilaya ya Kilombero ameuawa kwa kukatwa mapanga shingoni na ubavuni na
watu wasiofahamika huku chanzo kikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Shilogile alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 27 mwaka huu katika Tarafa ya Mlimba Wilaya ya Kilombero.
Huko maeneo ya mashamba ya Agrofocus Kata ya
Magomeni Wilaya ya Kilosa, mtu ambaye hakufahamika amekutwa amekufa na
mwili wake ukining’inia kwenye mti baada ya kujinyonga.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment