Home » » Wafugaji sasa watishia kufunga mnada Dumila

Wafugaji sasa watishia kufunga mnada Dumila

Kilosa. Migogoro ya ardhi wilayani Kilosa, Morogoro, itaikosesha mapato halmashauri ya wilaya hiyo, baada ya wafugaji kuazimia kutouza mifugo yao kwenye mnada mkubwa wa mifugo wa Dumila na badala yake kuhamishia shughuli hizo huko Mikongeni katika Barabara ya Morogoro-Dodoma, wilayani Mvomero.
Hayo yalibainishwa juzi katika mjadala wa mafunzo kwa viongozi wa serikali, dini taasisi na wanachi, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Greenbelt School Trust Fund (GSTF) The Foundation for Civil Society.
Wakizungumza kwenye mjadala huo, Ibrahim Poromoka wa Kitete na Michael Kashu wa Ngoisani- Mabwegere, walielezea wasiwasi wao kuhusu kuporomoka mara dufu, mapato ya Halamashauri ya Kilosa kama hakutakuwa na hatua madhubuti za kulikabili tatizo hilo.
“Migogoro ya ardhi ni mingi ukiwamo wa wakulima na wafugaji, mipaka baina ya vijiji na vijiji na ile ya mtu na mtu lakini kubwa hapa ni wenzetu wafugaji kuikosesha mapato Serikali ya wilaya Kilosa kwa kuua Mnada wa Dumila na kwenda kuendeleza Mnada wa Mkongeni wilayani Mvomero,” alisema Poromoka.
Alisema bila kujali kuwa mnada huo una manufaa makubwa kwao na Serikali ya wilaya hiyo. Wafugaji hao jamii ya Kimasai, wameamua kutouzia mifugo yao kwenye mnada huo wa Dumila.
Kashu ambaye ni mfugaji wa jamii ya Kimasai, alisema uamuzi wa kuhamishia shughuli zao katika mnada wa Mkongeni, umefanywa na mikutano ya mila na makundi mbalimbali ya jamii hiyo wakiwamo Morani.
“Hakuna mtu anayependa ugomvi, kisa cha wafugaji kuhama Mnada wa Dumila na kwenda Mkongeni ni vurugu zilitokea Machi mwaka huu na kusababisha barabara kuu kufungwa,” alisema Kashu.
Alisema baada ya tukio hilo, makundi ya kimila ya Wamasai yalikutana na kujadili hali iliyojitokeza na hatimaye kuhamisha Mnada wa Dumila.
Hata hivyo Katibu wa GSTF John Mengele na ofisa tarafa hiyo ya Magole Moses Nchimbi waliwataka viongozi wa serikali za vijiji na kata kufanya kazi ya ziada kutatua migogoro mapema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa