CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Kilosa,
kimefunga mwaka huku kikiitaka serikali wilayani humo kujipima na
kujitathimini kama imefanikiwa kutawala kwa maendeleo.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika mjini hapa juzi, Mwenyekiti wa
CHADEMA Kilosa, Seleman Simba, alisema umasikini walionao wananchi
unatokana na mfumo mbovu wa utawala ndani ya serikali.
Udhaifu huo alioutafsiri kuwa unatokana na kuogopana kinafiki kwa
lengo la kulindana, ulisababisha maafa makubwa baina ya wananchi
wilayani humo na kuendeleza wimbi la umasikini usiotarajiwa kutokana na
hali ya hewa na ardhi.
“Ni nani hapa nchini na nje ya nchi hafahamu kuwa Kilosa ndiyo wilaya
pekee ya mfano wa migogoro ya ardhi? Si chini ya watu watatu wanakufa
kila wiki kutokana na migogoro hii, lakini nani na kwa mbinu gani
ameshituka kukomesha hayo?” alihoji Simba.
Alisema nchi imejaa sheria za ardhi zisizotekelezeka, na kusisitiza
kuwa sheria hizo zitaendelea kuchakaa kwenye makabati ya serikali hadi
hapo nchi itakapopata viongozi kutoka vyama vingine ikiwemo CHADEMA.
Awali, Mhamasishaji wa Kanda, Shabani Dimoso, alisema bado serikali
haijawa na dhamira ya kukomesha wizi na ufujaji wa mali na fedha za
umma akitoa mfano kwenye halmashauri hiyo kuendelea kupata hati chafu.
“Wananchi wasiogope na kutishwa na mamlaka iliyopo kwa kuwa wanachopigania ni haki yao kikatiba,” alifafanua Dimoso.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment