Ulanga. Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti
amesema kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera
kuchunguza chanzo cha vurugu zilizosababisha mauaji ya wakulima watatu
wanaodaiwa kuuawa na polisi katika Kijiji cha Igawa, Kata ya Malinyi,
Ulanga imeanza kufanya kazi na kwamba hali ya usalama na amani imerejea.
Akizungumza jana mjini hapa Miti alisema baada ya
tume hiyo kukamilisha uchunguzi wake, wananchi watapewa taarifa ya
chanzo cha vurugu hizo zilizotokea baada ya wananchi kuvamia Kituo cha
Polisi Malinyi na kufanya uharibifu.
Alisema wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi
yake, Jeshi la Polisi limewahamisha baadhi ya askari wa kituo hicho
akiwamo mkuu wake ili kuleta imani.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema uamuzi wa kuwahamisha
askari hao ulikuja baada ya baadhi ya wananchi, hususan wakulima
kutokuwa na imani nao.
Alisema baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya kufanya vikao na mikutano ya hadhara, wakulima na wafugaji
walikubaliana na kuunda kamati ya pamoja kila upande ukiwa na
wawakilishi watano ili kuimarisha amani na usalama.
Alisema hivi sasa wananchi wanaendelea na shughuli
zao za kiuchumi na kijamii na kuwataka viongozi wa eneo hilo kuwa
mstari wa mbele kurejesha amani badala ya kuchochea vurugu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment