Home » » Wakulima wamjia juu Waziri wa Mifugo

Wakulima wamjia juu Waziri wa Mifugo

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Dk. Mathayo David
 
Ng'ombe 360 wa mfugaji Makweru Shega nusura izushe tafrani baada ya  Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David kujaribu kuwashawishi wananchi na viongozi wa halmashauri wampunguzie adhabu na fidia mfugaji huyo ili aondoe mifugo yake iliyokuwa ikishikiliwa kuinusuru kufa na kiu na njaa.
Waziri Mathayo aliwasili katika kijiji cha Bwila Chini, Kata ya Serembala juzi na moja kwa moja kwenda katika eneo lililokuwa limetengwa maalum kuwakusanya mifugo ya wafugaji wanaodaiwa kuwa wavamizi.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri huyo alielezwa uwapo wa  ng’ombe wa mfugaji, Makweru Shega, kama kundi mojawapo lililokamatwa katika operesheni ondoa mifugo iliyoanza kutekelezwa wilayani Morogoro, wakidaiwa kutokea mkoa  jirani wa Pwani kuelekea katika kijiji cha Duthumi bila kibali.

Wananchi hao walieleza walilazimika kuwashikilia ng’ombe hao hadi mmiliki wake atakapolipa faini ya Sh. 50, 000 kwa kila ng’ombe sawa na Sh. milioni 15 kwa ng’ombe wote na kwamba kadiri siku zinavyoongezeka alitakiwa kuongeza shilingi elfu kumi zaidi kama tozo ya kutunziwa mifugo yake na akishindwa ipigwe mnada.

Kitendo hicho kilimgusa Waziri huyo mwenye dhamana ya mifugo na kuwataka wananchi hao wamuachie mfugaji huyo kwa kulipa faini ya Sh. 10, 000 kwa kila ng’ombe ili kunusuru kufa kutokana na kiu na njaa.

‘”Hili sasa ni agizo, waachieni hawa ng’ombe waende na mifugo ilipiwe Sh. 10,000 kwa kila mmoja, mmeshawashikilia kwa siku ya sita sasa, wanazidi kukonda na hata wengine kufa, na hata mkiuza hamuwezi kupata thamani kubwa kama mnayotaka ilipiwe faini, ni kweli mnasimamia sheria, lakini fanyeni na ubinadamu pia” Waziri huyo aliwaambia wananchi hai hao. Hata hivyo, Waziri huyo alijikuta katika wakati mgumu baada ya kupigwa vikali na wananchi na viongozi wa kijiji hicho.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Yasini Msangi, alilazimika kutoa ufafanuzi wa sheria inayotumika katika operesheni hiyo, ambayo iliundwa baada ya kuwapo kwa migogoro ya muda mrefu ya wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo.

Alieleza kwamba, sheria hiyo inasema iwapo mfungaji ameshindwa kukomboa mifugo yake kwa muda uliopangwa, mifugo iliyokamatwa inachukuliwa hatua ya kupigwa mnada.

Alisema wameamua kuweka tozo hiyo na nyongeza ya gharama kadiri mifugo itakavyozidi kushikiliwa, kutokana na operesheni hiyo kugharimu fedha nyingi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bwila Chini, Mohamed Kinyogoli na wananchi wake, pamoja na viongozi wengine wa kata na Chama cha Mapinduzi walipingana na maamuzi ya Waziri ya kutaka kupunguzwa kwa adhabu.
Walisema kitendo hicho ni cha kuwapendelea wafugaji kwa makusudi, kwani hakuna anayewatetea wakulima wakipigwa ama kuuawa na makundi ya wafugaji wavamizi katika maeneo yao, matukio ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.

Hata hivyo, Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi aliwataka wakulima na wafugaji kuishi kama ndugu bila kujengeana chuki na visasi miongoni mwao na kila mmoja kuheshimu mipaka ya mwenzake, kwani mifugo haipaswi kula mazao ya wakulima na wakulima hawapaswi kuitesa mifugo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa