Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera
Makamu mwenyekiti wa chama cha wafugaji nchini, Kipalenei Kifutu, alisema kuwa amewapatiwa taarifa za watu watano kufariki katika mapigano hayo wakiwemo wafugaji wawili na wakulima watatu.
Alisema pia kuna idadi kubwa ya majeruhi ambao wengine wamejeruhiwa kwa mishale na wengine kupigwa na mapanga na wamelazwa katika Hospitali ya Bwagala.
“Pia nimepokea taarifa kuwa watu waliosababisha mapigano hayo wametokea wilayani Gairo na kufika katika kijiji cha Kambara wakidai wao ndiyo wakulima wa mashamba hayo na kukamata ng’ombe 300 za wafugaji huku zingine wamechinja na wengine wamewakata kata tu jambo lilofanya kutokea kwa mapigano haya,” alisema.
Aidha alisema mapigano hayo yalianza tangu juzi, lakini polisi wamefika jana katika kijiji hicho majira ya saa sita.
“Wakulima wamechukua hizo ng’ombe, lakini DC (Mkuu wa Wilaya) Mvomero kaombwa msaada akawa anatoa kauli za kuchochea akidai kuwa wafugaji waende kufuata ng’ombe zao kwa wakulima na wakienda wakulima wanaambiwa kachukueni ng’ombe kwa wafugaji kwani wao wamezoea kulisha katika mashamba yenu...kauli kama hii imesababisha watu kupigana tu mpaka muda huu,” alisema Kifutu.
Mkazi mmoja wa kijiji hicho, Fabiano Hamza, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Mvomero akisema kuwa mapigano hayo yamesababisha shule kadhaa za msingi zilizoko eneo hilo pamoja na Shule ya Sekondari ya Embeti kufungwa kutokana na mapigano hayo.
Alisema kuwa baadhi ya wazazi wamelazimika kuwahamishia watoto wao katika shule za maeneo mengine akiwamo mdogo wake ambaye alisema amehamishiwa katika shule moja ya Dakawa.
Alisema kuwa hali hiyo inawaathiri zaidi watoto wa sekondari kwa kuwa mitihani ya kidato cha nne iliyoanza Jumatatu inaendelea. Aliongeza kuwa juzi kuna mkulima mmoja ambaye juzi alipigwa risasi ya tumboni na wafugaji na kwamba jana zilipatikana habari kwamba alifariki dunia.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alipoulizwa jana, alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, kwa maelezo kuwa alikuwa katika eneo la tukio.
Hata hivyo, Shilogile kila alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani ilikuwa inapokelewa na msaidizi wake akisema kuwa bosi wake alikuwa katika vikao eneo la tukio.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment