Home » » Wakulima Mvomero wawaweka kati mawaziri mkutanoni

Wakulima Mvomero wawaweka kati mawaziri mkutanoni

Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel Nchimbi
 
Mawaziri  watatu na Naibu Waziri mmoja waliojitosa kwenda kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji uliopelekea vifo vya watu sita  katika vijiji vya Hembeti na Kambala wilayani Mvomero, wamejikuta katika wakati mgumu baada ya wakulima kuwabana na kuhoji walikuwa wapi kabla ya kutokea kwa vifo hivyo na wengine watu kujeruhiwa.
Mawaziri waliokumbana na zahama hiyo ni, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David, Waziri wa Kilimo na Chakula Mhandisi Christopher Chiza, Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Ole Medei.

Mawaziri hao  walijikuta wakibanwa na wakulima wanaolima katika Bonde la Mgongolwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mkindo, tarafa ya Tuliani ulioitishwa kwa ajili ya kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ambao wiki iliyopita ulisababisha vifo vya watu sita baada ya kutokea mapigano.

Katika mkutano huo wakulima walianza kuitupia lawama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kutokana na kushindwa kutoa maamuzi juu ya uhalali wa wakulima ambao wamekuwa wakilima kwa muda mrefu katika bonde hilo licha ya kuwasilisha maombi yao mbalimbali na baadaye kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Ardhi.

Akitoa malalamiko hayo kwa niaba ya wenzake, mkulima Boniface Kizimbali, alisema endapo suala lao lingepatiwa ufumbuzi mapigano hayo yasingetokea na kusababisha vifo hivyo.

Alisema kutokana na kuchelewa mpaka suala hilo kupelekwa mahakamani kumejenga kiburi kwa baadhi ya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba yao kwa madai yapo katika eneo lao huku wakulima wakiendelea kupata hasara.

Akijibu, Naibu Waziri Medei alisema wizara ilianza kuyafanyia kazi madai hayo ya wakulima lakini baadaye suala hilo likafikishwa mahakamani hivyo kwa sasa ameshamuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha shauri hilo linasikilizwa haraka.

Naye Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alishangazwa na mamlaka zilizopo wilayani humo kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa wakulima kwa kuchelewesha kutoa majibu na kupelekea mazao kuliwa mashambani  na kusababisha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Hata hivyo alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wakulima wa bonde hilo la Mgongolwa na kuwataka kuwa wavumilivu mpaka shauri hilo litakapopatiwa ufumbuzi Mahakama Kuu.

Naye Abubakar Hussein mkazi wa Hembeti alimshushia lawama  Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuwa ameshindwa kuwawekea utaratibu wafugaji na kusababisha wafugaji kulisha mifugo kwenye mashamba yao kutokana na kutowajengea majosho ya kunyweshea mifugo yao.

Akijibu, Waziri Dk. Mathayo alikiri kukosekana kwa miundombinu ikiwamo ya majosho na malambo katika maeneo ya wafugaji hali ambayo imechangia wafugaji kulishia katika mashamba na kusema kuwa tayari serikali imeshajipanga kuwajengea wafugaji miundombinu hiyo katika sehemu zao walipo ili kutatua tatizo hilo la wakulima na wafugaji.

Naye Veronica Joseph alielekeza lawama kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa askari wa Jeshi Polisi hawakutenda haki baada ya kutokea mapigano hayo kutokana na kuwakamata wakulima 30  na wafugaji wawili tu katika vurugu za Novemba 4 na 5 wakati vifo vya wakulima vilikuwa vinne na wafugaji vilikuwa  viwili.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Nchimbi alimjia juu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustini Shilogile na kueleza kuwa hajaridhishwa na ukamataji wa watuhumiwa hao wa vurugu hizo na kuagiza kuwaachia huru wasio na hatia.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa