MAWAZIRI watatu; Injinia Chritopher Chiza wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Prof. Anna Tibaijuka wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na Dk. Mathayo David wa Mifugo na Uvuvi, wamejitosa wilayani
Mvomero mkoani Morogoro kutanzua mgogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Mapigano hayo yalitokea kati ya Novemba 5 na 6 mwaka huu na
kusababisha vifo vya watu sita, huku wengine zaidi ya 50 wakijeruhiwa
vibaya katika Kata ya Hembeti wilayani Mvomero.
Kwa mujibu wa diwani wa kata hiyo, Juma Malaja, mawaziri hao
walitarajia kupokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi juu ya
mgogoro huo na nini kifanyike ili kuumaliza.
Alisema kabla ya mkutano na wananchi katika kijiji hicho cha Hambeti,
mawaziri hao walitarajia kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya chini ya mkuu wa wilaya hiyo, Anthon Mtaka, kwa taarifa fupi ya
maendeleo na hatima ya mapigano hayo.
Hata hivyo, wakati viongozi hao wakijaribu kutafuta muafaka wa tatizo
hilo kwa kuwakutanisha wafugaji na wakulima, Jeshi la Polisi na
viongozi wa serikali wilaya na mkoa, wanadaiwa kuhusika katika vurugu
hizo.
Madai hayo ya viongozi kuhusika yalikanushwa na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, akisema ni maneno ya wapita njia.
Kwa mujibu wa Diwani Mjala, jioni ya Novemba 4, wanakijiji walikamata
ng’ombe wasiopungua 300 wakiwa wameharibu chanzo cha maji na kula
mazao ya watu mbalimbali mashambani.
Alisema kuwa alipopewa taarifa za kukamatwa kwa mifugo hiyo, alitoa
taarifa kwa OCD na mkuu wa wilaya hiyo, akiomba msaada zaidi wa
kiulinzi ili waimarishe ulinzi kutokana na tabia za wafugaji zilivyo,
kuwa kungeibuka mapigano muda wowote.
“Baada ya kukamatwa kwa ng’ombe wale, mimi niliamua kutoa taarifa kwa
viongozi wa juu, lakini pia kuomba kuongezewa nguvu ya ulinzi maana
kama wanavyofahamika wafugaji, wasingevumilia mifugo yao ilale nje,
lakini mpaka Novemba 5, hakuna askari aliyekuwa amefika,” alisema
Malaja.
Aliongeza kuwa saa 12 jioni ya Novemba 6, walipelekwa askari ambao
hawakufanya lolote kutokana na mazingira ya mapambano kuwa magumu
kutokana na aina ya silaha zilizokuwa zikitumika na muda kuwa umeisha.
Vurugu hizo zilizimwa na Kamishina wa Operesheni Makao Makuu, Paul
Chagonja aliyeingia eneo la tukio huku watu sita wakiwa wamepoteza
maisha na wengine wengi kujeruhiwa vibaya.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment