Home » » RUBADA yawataka maofisa ugani kuwa wabunifu

RUBADA yawataka maofisa ugani kuwa wabunifu

MAMLAKA ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imewataka maofisa ugani katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kuwa wabunifu katika utendaji wao ili kuongeza thamani ya mazao pamoja na kutoa elimu stahiki kwa wananchi wanaowatumikia.
Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Aloyce Masanja, alitoa ushauri huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, mkoani hapa wakati wa semina elekezi kwa watendaji wa halmashauri hiyo juu ya mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hivi karibuni.
“Ni vema maofisa ugani wakaelewa kuwa wao ndio viongozi katika suala la kutoa maelekezo kwa wananchi wao,” alisema.
Alisema maofisa ugani waliopo ni wachache kulinganisha na mahitaji yaliyopo katika vijiji, hivyo kazi kubwa iliyopo ni kujaribu kuwapa elimu ili waendane na mfumo uliopo na mahitaji ya wakati.
“Tumekuwa na wagani wachache katika vijiji, japo wanafanya kazi lakini wamekuwa si mfano bora kwa wale wanaowatumikia, kutokana na wao wenyewe kutojishughulisha na kilimo na ndiyo maana hata wananchi wamekuwa na hamasa ndogo juu ya suala la kilimo,” alisema Masanja.
Aliongeza kuwa utakuta ofisa ugani hana shamba au mfugo, jambo linalosababisha wao wenyewe kutokuwa na mwamko katika sekta ya kilimo na mifugo katika vijiji wanavyofanyia kazi.
Akizungumzia upungufu wa maghala ya chakula katika Wilaya ya Morogoro Vijijini, Masanja alisema tatizo hilo linatokana na kuwepo kwa maghala ya zamani ambayo hayana viwango vya kuweza kuhifadhi chakula.
“Katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa tunataka kila kijiji kiwe na kilimo cha umwagiliaji na patajengwa ghala la kisasa kwa ajili ya kuhifadhia chakula,” alisema.
Alisisitiza kuwa sasa kuna upotevu mkubwa wa chakula hasa mpunga na mahindi kutokana na kutohifadhiwa katika maeneo maalumu, hivyo kusababisha njaa zisizokuwa za lazima katika maeneo kadhaa ya wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Saidi Amanzi, alisema serikali ina nia nzuri ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi, hivyo ni vema wakaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali yao.
“Sisi upande wa serikali tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la kilimo chenye tija na kitakachomkomboa mwananchi,” alisema Amanzi.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa