MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Lugala maarufu kama machimbo ya
mchanga mweupe mjini Morogoro, Willison Mizola (CHADEMA), amenusurika
kufa baada ya kuvamiwa na kupigwa na watu aliodai kuwa wafuasi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza kwa tabu na mwandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa
mkoani Morogoro alipolazwa kwa matibabu, Mizola ambaye ni mwenyekiti
pekee katika Manispaa ya Morogoro kupitia upinzani, alisema tukio hilo
lilitokea Novemba 28 wakati akielekea kwa rafiki yake Mtaa wa Lugala,
Kata mpya ya Mindu.
Alisema siku ya tukio, akiendesha pikipiki katika maeneo ya korongo
jirani na machimbo hayo, alizingirwa na kundi la watu wakiwa na aina
mbalimbali za silaha za jadi kisha kumpiga nazo sehemu za mwili jambo
lililomsababishia kupoteza fahamu na kuanguka chini.
“Waliponiona nakuja, nikasikia wakisema kwa sauti ‘huyo ndiye tunayemtafuta muda mrefu sasa amepatikana’.
“Pale kulikuwa na mitambo ya kupakilia mchanga kwenye magari, na
miongoni mwa waliokuja kinishambulia ni pamoja na wale wenye mtambo
huo,” alisema Mizola.
Alisema baada ya kuona amepoteza fahamu, watu wale hawakutaka
kuchukua ile pikipiki ila walimpora sh 1,360,000 alizokuwa akirejesha
kwa mdeni wake.
“Baada ya muda nilizinduka na kufanikiwa kuinua pikipiki na kuiwasha
kisha nikaondoka eneo hilo hadi kwa rafiki yagu niliyekuwa naenda kwake
ambaye alinikimbiza kituo cha polisi na kupata PF3 kwa ajili ya
matibabu,” alisema.
Mizola alisema kuwa aliambiwa kuwa mishipa miwili ya damu shingoni imefyatuka na kuyumba.
Aliwataja baadhi ya vijana aliowatambua kuhusika na tukio hilo kuwa
ni Komu Adam, Omary, Torati Mathias, Athuman Malolo, Elistini Msumle,
Israel Mganda na Victor Mkude wote wakazi wa Mtaa wa Lugala.
Kamanda wa Polis Mkoa wa Morogoro, Faustin Shilogile amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba Mizola amefungua jalada la shambulio
namba MOR/IR/6697/13 na IR/12981/13 lakini hadi sasa hakuna
aliyekamatwa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment