Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ni
mamlaka iliyoanzishwa kwa Amri ya Serikali na kutangazwa kwenye gazeti la
Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei,
2014. Uanzishwaji wa Mamlaka hii ni utekelezaji wa kifungu cha 8 cha Sheria ya
kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Mamlaka
ya Wanyamapori imeanza kazi rasmi tarehe 1 Julai,2016 na Makao Makuu kwa sasa yapo hapa Morogoro katika eneo la
Taasisi ya Utafiti wa mazao ya Misitu (TAFORI).
TAWA
inasimamia Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 42, maeneo manne (4) ya Ardhioevu
yanayotambuliwa na Mkataba wa kimataifa wa Ramsar pamoja na maeneo ya wazi
yenye wanyamapori. Aidha, TAWA ni muangalizi wa shughuli za uhifadhi
wanyamapori kwenye maeneo ya Jumuiya za Uhifadhi za Wanyamapori kwa jamii
(Wildlife Management Areas).
Mamlaka
inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007,
Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake. Vilevile,
Mamlaka inatekeleza mikataba ya kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na
mazingira yao ambayo Tanzania imeridhia. Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi
nyingine za uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu inatekeleza Mkakati wa kupambana
na Ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali wa miaka mitano
(2014-2019).
Mamlaka
ilianzishwa kama chombo cha utekelezaji wa majukumu kwa niaba ya Serikali chini ya uangalizi wa
Serikali na kuwa na mfumo unaonesha
utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi. Kama ilivyo kwa Mamlaka nyingine
nchini, lengo la kuanzishwa kwa TAWA, ni kutekeleza majukumu ya Idara ya
Wanyamapori hasa ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini. Ikiwa ni pamoja na
kusimamia shughuli za utawala, ulinzi na usimamizi wa raslimali ya Wanyamapori
katika maeneo yote nje ya Hifadhi za Taifa na eneo ya Ngorongoro. Hii ni pamoja na kutekeleza
kazi zifuatazo;
Kusimamia
Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu, Kusimamia na kulinda shoroba za wanyamapori,
maeneo ya mtawanyiko, ardhioevu, na maeneo ya wazi yenye wanyamapori, Kuangalia
Usimamizi wa wanyamapori katika Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori,
Mashamba na Bustani za wanyamapori kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na
Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Kusimamia
migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kwa kushirikiana na wadau wengine wa
uhifadhi, Kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wananchi katika kuanzisha na
kusimamia uwekezaji katika maeneo ya wanyamapori, Kutoa, kurejea au kufuta
vibali vya matumizi ya wanyamapori, Kusimamia himasheria na kukabili ujangili. Kueleimisha
wadau kuhusu thamani ya wanyamapori.
Kushirikisha
wadau katika kuhifadhi na kunufaika na raslimali ya wanyamapori nchini,
Kushiriki katika Utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa Kusimamia
masuala ya utawala bora katika Usimamizi wa wanyamapori na Kuendeleza na kujenga uwezo wa Mamlaka katika Usimamizi wa
wanyamapori.
Moja
ya sababu ya kuanzishwa TAWA ni uwezo mdogo wa utendaji wa idara ya wanyamapori
uliotokana na uchache wa rasilimaliwatu, fedha na vitendea kazi.
Mafanikio
Katika
kipindi cha Julai 2016 hadi Octoba 2017, Mamlaka iliendelea kuimarisha Ulinzi
wa rasilimali ya Wanyamapori ndani na nje ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na
maeneo ya Ardhioevu (Ramsar Sites). Muundo wa usimamizi na ulinzi wa rasilimali
za wanyamapori katika Mamlaka umegawanywa katika makundi makuu mawili. kundi la
kwanza linahusisha mameneja wanaosimamia mapori ya akiba 28 na “Ramsar Sites”
3; na kundi la pili ni wakuu wa kanda 8 wa Kikosi Dhidi Ujangili (KDU).
Mamlaka
inashirikiana na Halmashauri za Wilaya na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori
(WMAs) katika ulinzi na usimamizi wa wanyamapori kwenye mapori Tengefu, maeneo
ya wazi na udhibiti wa wanyamapori hatari kwa maisha ya binadamu na waharibifu
wa mali za wananchi.
Kiujumla TAWA imefanikiwa kutekeleza mambo
yafuatayo
Kuimarisha
usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na kuboresha uwezo wa kukusanya
maduhuli, Mamlaka imeendeleza mfumo wake wa kukusanya mapato kwa kutumia mfumo
wa kielektronic ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato.
Kutokana
na mabadiliko ya mfumo wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi .TAWA imeanza kuendesha mafunzo ya maandalizi ya kuingia
Jeshi usu (Paramilitary) katika kambi ya Mlelele iliyoko Katika Pori la Akiba
Rukwa/Lwafi Mkoani Katavi. Mafunzo haya pia yanashirikisha askari kutoka Hifadhi
za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Tangu mafunzo haya yaanze
tumeshapeleka Askari zaidi ya 260 ambao wameshahitimu na sasa sasa hivi kuna
askari 60 wanaendelea na mafunzo hayo.
TAWA
kupitia Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt John Pombe Joseph
Magufuli, imeendelea kukabiliana na ujangili kwa nguvu zote kwa njia mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kutekeleza Mkakati wa kupambana na ujangili na biashara
haramu ya nyara za Serikali (National Antipoaching Strategy to Combat Poaching
and Illegal Wildlife Trade) iliyozinduliwa Novemba, 2014.
Doria na intelijensia ndani na nje ya maeneo
yaliyohifadhiwa zinaendelea kufanyika nchi nzima.
Serikali
kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa
zikiwemo taasisi za kikanda na kimataifa, imefanya jitihada mbalimbali
kukabiliana na ujangili wa tembo. Zimeonekana dalili za kupungua kwa ujangili
wa tembo nchini kutokana na jitihada kubwa ya kuimarisha doria za kupambana na
ujangili hali hiyo imesaidia kukamatwa kwa silaha nyingi zilizokuwa zikitumika
kwa ujangili.
Jumla ya watuhumiwa 2,053
walikamatwa kwa makosa mbalimbali na kufunguliwa mashitaka ambapo jumla ya kesi
859 zilifunguliwa. Kesi 10 + 126 zenye watuhumiwa 248 zilihukumiwa kifungo cha
jumla ya miezi 8,295 na kesi 198 zenye watuhumiwa 234 watuhumiwa walilipa faini
jumla ya shilingi 387,985,063/=.
Nyara za aina mbalimbali
zilikamatwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2016 hadi Oktoba 2017 kama
ifuatavyo; Meno ya tembo vipande 848 vyenye uzito wa kilo 2,664.48, Nyamapori yenye uzito wa kilo 7,790 za spishi
mbalimbali na Meno 8 ya kiboko, magunia 67 ya magamba ya kakakuona, ngozi 16,
na mikia 33 ya wanyamapori mbalimbali.
Mwezi Julai,2016 kilianzishwa
Kikosi Kazi kiitwacho’ Wildlife and Forest Crime Unit – WCU’ kinachosimamiwa na
Watendaji wa Sekta ya Wanyamapori kupitia Kanda za Kiikolojia tisa, (Tasking
and Coordination Groups – TCGs) ili kukabiliana na majangili katika ngazi za
juu za uwezeshaji (Facilitators) ambacho kinashirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama kupitia Muungano wa Kitaasisi.
TAWA inaamini kwamba
changamomoto za ujangili na uvunaji haramu wa misitu na matatizo mbalimbali
yanayohikabili uhifadhi nchini hayawezi kutatuliwa kwa mfumo wa utendaji kazi
wa kiraia. Hivyo, Wizara inakamilisha taratibu za kubadili mfumo wa utendaji kazi
kutoka wa kiraia kwenda jeshi usu.
Mabadiliko haya ya kimfumo
ni matakwa ya Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 ambayo
imeanisha kwamba kutaundwa kikosi cha jeshi usu (Wildlife Protection Unit), ili
kuhakikisha ulinzi kamili wa rasilimali katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Katika kipindi cha mwezi
Agosti hadi Oktoba, 2016 kikosi kazi hiki, kimefanikiwa kukamata majangili 107, kesi 9 ziko mahakamani, Aidha, nyara,
silaha, vifaa mbalimbali vya kufanyia
ujangili vimekamatwa.
Ukaguzi wa nyara umeimarishwa
katika viwanja vya ndege na bandari kwa kutumia mbwa maalum wa kunusa ili
kutambua nyara na kufuatilia majangili.
Doria imeendelea kufanyika
kwa kutumia ndege zisizotumia marubani ‘Drons’ kukabiliana na ujangili.
Elimu
ya uhifadhi ni nyenzo muhimu katika kupambana na ujangili pamoja na uharibifu
wa mazingiara. Mamlaka kwa kutambua umuhimu wa dhana nii, imetoa elimu ya
uhifadhi kwa vijiji (45) vinavyozunguka Pori la Akiba Selous, vijiji (19)
kuzunguka Pori la Akiba Rungwa/ Muhesi/Kizigo ,Tengefu na maeneo ya wazi ambayo
ni vitalu vya uwindaji wa kitalii.
Aidha,
wananchi walielimishwa kwa njia ya
runinga,redio,magazeti na kugawa vipeperushi kwa wananchi katika maonesho ya
Sabasaba, nane nane, siku ya utalii duniani,siku ya tembo, siku ya wanyamapori
duniani na siku ya ardhioevu duniani. Majarida 585, Vipeperushi 7000, Stickers
3000, Mabango 5 yenye ujumbe wa uhifadhi vimegawiwa kwa wananchi.
Ushirikishwaji wa jamii
katika uhifadhi wa Wanyamapori uliimarishwa kwa kutangazwa eneo la Jumuiya la
Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Area-WMAs) Ngorongo, Utete na
Mwaseni (JUHIWANGUMWA) lililoko katika Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani
lilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GN. Na 204 la tarehe 01/07/2016) na
kufanya jumla ya maeneo yaliyotangwazwa kuwa 22.
Kushirikiana na nchi jirani
(Cross border collaboration) kutanzua changamoto za uhifadhi, ujangili na
biashara haramu. Katika eneo hili Tanzania inashirikiana na Msumbiji, Zambia,
Uganda na Kenya kukabili ujangili unaovuka mipaka ya nchi.Hivyo, Kutokana na
hali mizoga ya tembo imeonekana na meno ya tembo kukamatwa.
Changamoto
Mamlaka
ya Wanyamapori bado ni Mamlaka mpya. Mamlaka
katika kufanya kazi zake imekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za
ujangili,mwamko mdogo wa Watanzania kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo
mapori ya akiba; ubovu wa miundombinu katika maeneo yaliyohifadhiwa, shughuli
za kibinadamu hususan kilimo na uingizaji wa ng’ombe katika katika maeneo
yaliyohifadhiwa na matumizi haramu ya wanyamapori.
Ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo
Bado imeendelea kuwa
changamoto ya kiuhifadhi. Hali hii
inaathiri siyo tu kuuawa kwa wanyamapori, bali pia inahatarisha utalii na
usalama wa nchi yetu. Sensa ya mwaka 2014 iliyofanyika nchi nzima ilionyesha
kwamba idadi ya tembo nchini ni 43,330 ikionyesha kupungua kwa idadi ya tembo
kutoka tembo 109, 051 mwaka 2009, Sawa na asilimia 60.3% ya kupungua kwa idadi
ya tembo katika kipindi cha miaka mitano. Pia matokeo ya sensa ya mwaka 2014
yalionyesha ongezeko la asilimia 16% la idadi ya tembo katika mfumo wa Ikolojia
wa Selous-Mikumi kwa kufikia 15,217 kutoka 13,084 iliyokuwa mwaka 2013. (Chanzo:Sensa za TAWIRI.)
Mapito/Shoroba za Wanyamapori
Zinaendelea kuzibwa na
uvamizi wa mifugo/shughuli za binadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa. Hali hiyo
imesababisha kuongezeka kwa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori na
kupungua kwa idadi ya wanyamapori hususani tembo ndani na nje ya maeneo
yaliyohifadhiwa.
0 comments:
Post a Comment