WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali katika wizara
hiyo, kutumia fedha kulingana na miongozo ya serikali na si kugawana kwa
kulipana posho za nyumba, vikao na safari za nje kinyume na taratibu na
maelekezo ya serikali.
Profesa Ndalichako alisema hayo juzi mjini Morogoro, wakati akifungua
mkutano wa viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ambao
umelenga kuchanganua viashiria hatarishi katika sekta ya elimu na namna
ya kuboresha utekelezaji wa mifumo ya viashiria hivyo katika maeneo yao
ya kazi ili kukuza na kuendeleza elimu nchini.
Waziri huyo alisema kuwa; “Baadhi ya changamoto zinazoikumba taasisi
zilizopo chini ya wizara yangu ni ukosefu wa maadili, upungufu wa
wataalamu, vifaa, miundombinu zinazosababishwa na baadhi ya viongozi
kutumia fedha kinyume na utaratibu.”
Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na tabia kwa baadhi ya viongozi wa
taasisi za wizara hiyo, kuona kuwa taasisi hizo haziko chini ya serikali
na kutofuata miongozo ya utumishi wa umma. Alisema wizara haina chanzo
chochote cha kuingiza mapato, hivyo ni wajibu kwa viongozi wa taasisi
mbalimbali katika sekta ziliz ochini ya wizara kutumia fedha kulingana
na miongozo ya serikali na si kugawana kiholela.
“Si vizuri kuendelea kujilimbikizia fedha za serikali, na ni vizuri
kutumia fedha hizo kulipa malimbikizo na madeni ya wafanyakazi pamoja na
kuwannulia vitendea kazi,” alisema Profesa Ndalichako.
Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk
Leonard Akwilapo kuandika mwongozo wa serikali ili watakaoukiuka
matumizi ya fedha za umma washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na hayo, aliwataka viongozi hao kuacha kuwasubiri viongozi wa
juu kufuatilia mikataba wanayoingia na wadau wengine badala yake wawe wa
kwanza wao kufuatilia miradi hiyo na kuisimamia Baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo, kwa nyakati tofauti, waliahidi kutumia mafunzo hayo na
kutekeleza maagizo ya waziri kwa lengo la kuleta ufanisi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment