Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius
Kahyarara alipotembelea shamba la kubwa la miwa linaloandaliwa ikiwa ni
sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama
Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya
NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika
gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko
wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio wakati wa ziara hiyo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) pamoja na Waziri wa Kazi, Ajira, Sera,
Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama (katikati) wakiongoza
zoezi la upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa
wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II
unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF
kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la
Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro. Kulia, akishirikiana nao ni Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akifuatilia kwa umakini maelezo kutoka kwa meneja
wa shamba hilo namna ambavyo miwa inapandwa kitalaam. Wengine ni pamoja
na Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista
Mhagama (kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe
(mwenye suti nyeusi).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akimshudia Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango akishiriki kwenye zoezi hilo.
Kisha
kazi ikaendelea…! Lengo ni kupanda ekari 3000 za miwa ifikapo Disemba
mwaka huu zoezi ambalo tayari limetoa ajira zaidi 150 kwa wakazi jirani
na eneo hili la Mbigiri na wengine kutoka mikoa jirani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine walipata fursa ya kusherehekea na wenyeji kupitia ngoma za asili.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (mwenye miwani) akisikiliza kwa umakini maelezo
kuhusu ubunifu wa michoro ya miradi mbalimbali kutoka kwa vijana wasomi
sita kutoka mikoa mbalimbali walioamua kuweka kambi kwenye eneo hilo
Mbigiri wakilala chini ya miti lengo likiwa ni kuunga mkono jitiahada za
ujenzi wa kiwanda hicho kwa kushiriki bila malipo katika hatua
mbalimbali za ujenzi wa kiwanda hicho ikiwemo kubuni mchoro uliotumika
katika moja ya jengo litakalotumika kujengwa kiwanda.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (alieshika jembe) akiongoza zoezi la upandaji wa
miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda
cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya
mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya
Mkulazi Holding unaofanyika katika gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani
Morogoro. Miongoni mwa wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Fedha na
Mipango Dk Phillip Mpango (alievaa suti nyeupe).
WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amepongeza hatua ya mifuko ya hifadhi ya jamii
hapa nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda huku akitoa wito kwa jamii
hususani vijana kuhakikisha wanaonyesha uzalendo kwa kujitolea kwa
vitendo kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kutatua tatizo la ajira
na kuinua uchumi wa taifa.
Waziri
Mkuu Majaliwa alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro mara tu
baada ya kuongoza zoezi la upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga
mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama
Mkulazi II unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya
NSSF na PPF kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika
gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani Morogoro.
"Pamoja
na kutoa pongezi kwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa
kuitikia vema wito wa serikali ya awamu ya tano katika uwekezaji wa
viwanda vyenye tija kwa taifa, kipekee nitoe wito kwa jamii hususani
vijana kuhakikisha wanaunga mkono jitahada hizi kwa kujitolea ujuzi na
maarifa katika kufanikisha adhma hii ya serikali inayolenga kuwanasua
kutoka kwenye uhaba wa ajira,'' alitoa wito.
Wito
huo wa Waziri Mkuu ulikuja kufuatia kuguswa na uzalendo ulioonyeshwa na
vijana wasomi sita kutoka mikoa mbalimbali walioamua kuweka kambi kwenye
eneo hilo Mbigiri wakilala chini ya miti lengo likiwa ni kuunga mkono
jitiahada za ujenzi wa kiwanda hicho kwa kushiriki bila malipo katika
hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwanda hicho ikiwemo kubuni mchoro
uliotumika katika moja ya jengo litakalotumika kujengwa kiwanda.
"Vijana
hawa ambao kwa sasa wamepatiwa maturubai ya kujihifadhi wamekuwa mfano
wa kuigwa na wenzao nchi nzima na nitazifikisha salamu zao kwa
muheshimiwa Rais ajue jitiahada zake zinatafsiriwa vyema sana na vijana
wazalendo wa taifa hili,'' alisisitiza.
Akizungumzia
mradi huo Waziri Mkuu alisema pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa
sukari hapa nchini, pia utapunguza tatizo la ajira sambamba na kukuza
uchumi wa nchi.
Ili
kuhakikisha wananchi wanakuwa kwenye nafasi ya kushiriki kikamilifu
katika kuzalisha malighafi kwa ajili ya kiwanda hicho Waziri Mkuu
aliutaka uongozi wa mkoa huo kuhakakikisha wanapita wilaya nzima ya
Kilosa unapotekelezwa mradi huo kuhakikisha hakuna mashamba pori zoezi
litakaloambatana na unyang'anyaji wa mashamba yasiyoendelezwa kutoka kwa
wamiliki wake na kisha kukabidhiwa kwa wananchi wayatumie kwa kilimo.
"Na
kwa wale wananchi wanaolima kwenye eneo la magereza utumike utaratibu
mzuri waweze kupata mashamba kwenye eneo la magereza waendelee na kilimo
hiki cha miwa ili kulisha kiwanda licha ya kuwa umiliki wa ardhi
utabaki kuwa ni wa jeshi la magereza,'' alifafanua.
Mradi
huo unaolenga kuzalisha tani 50 za sukari kwa mwaka ni sehemu ya mradi
mkubwa unaotekelezwa na mifuko hiyo katika eneo la Ngerengere, Wilaya ya
Morogoro Vijijini unaofahamika kama Mkulazi I ambao unaolenga kuzalisha
tani 200,000 za sukari kwa mwaka sambamba na kutoa ajira zaidi ya
100,000 katika hatua ya awali.
Kwa
upande wake Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu,
Jenista Mhagama alisema mifuko ya Hifadhi ya Jamii hapa nchini kwa
sasa inatekeleza miradi ya viwanda ipatayo 28 ambayo ipo katika hatua
mbalimbali kiutekelezaji lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais
Magufuli za kuwekeza katika uchumi wa viwanda.
Akionyesha
kuguswa na ushiriki wa wananchi katika mradi huo, Waziri wa Fedha na
Mipango Dk Phillip Mpango alimuahidi Waziri Mkuu kuwa anakwenda kutoa
maelekezo kwa Benki ya Kilimo nchini kuhakikisha inafika maeneo yote ya
mradi huo ili kuangalia namna benki hiyo inavyoweza kuwasaidia wananchi
kushiriki kikamilifu katika kilimo cha miwa.
Waziri
Viwanda, Biashara na Uwekezaji , Charles Mwijage alisema lengo la
serikali ni kuhakikisha taifa linazalisha sukari tani milioni mbili ili
lijitosheleze na kuunza nje ya nchi ambapo kwa sasa licha ya mahitaji ya
sukari kuwa ni tani 600,000 taifa linazalisha takribani laki tatu.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,
Prof Godius Kahyarara pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa
PPF, Bw.William Erio, walihakikishia serikali, wananchama na wadau wote
wa mifuko hiyo kuwa utekelezaji wa mpango huo pamoja na mambo mengine
unalenga kuongeza ajira na kupunguza kabisa kasi ya mfumuko wa bei kwa
kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.
"Tayari
mkandarasi wa kufunga kiwanda hiki ameshapatikana wakati zoezi la
upandaji wa miwa likiendelea. Lengo ni kupanda ekari 3000 za miwa
ifikapo Disemba mwaka huu zoezi ambalo tayari limetoa ajira zaidi 150
kwa wakazi jirani na eneo hili la Mbigiri na wengine kutoka mikoa
jirani,'' alisema Prof Kahyarara huku akiongeza mkuwa mradi huo pia
utazalisha umeme Megawatt 8 .
Naye
Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa alisema ufufuaji wa kiwanda
hicho kilichosimamisha uzalishaji wake katikati ya miaka 1990 mbali na
kuwa mchango mkubwa kwa jeshi hilo pia utatoa fursa kwa wafungwa
watakaoonyesha uwezo mkubwa katika utekelezaji wa mradi kuweza kupewa
nafasi ya kutumikia kiwanda hicho hata baada ya kumaliza vifungo vyao.
"
Kabla hakijasimamisha uzalishaji wake kutokana na changamoto kadhaa
ikiwemo uduni wa teknolojia na ukosefu wa vipuri kiwanda hiki kilikuwa
kinazalisha tani 8 hadi 10 za sukari kwa mwaka sasa kinakwenda kuzalisha
tani zipatazo 50 kwa kipindi hicho...kiukweli tunawashukuru sana NSSF,
PPF na serikali ya awamu ya tano,'' alipongeza.
0 comments:
Post a Comment