WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wale wote waliobinafsishiwa
viwanda vya umma mkoani Morogoro, kuhakikisha vinafanya kazi na si
vinginevyo na vikitumia malighafi ya ndani itokanayo na mazao ya kilimo
kwa lengo la kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Pamoja na kuwataka waliopewa viwanda kuviendeleza, pia amewataka
wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini kufanya hivyo kwa kuwa serikali
tayari inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Waziri Mkuu alitoa mwito huo juzi akiwa mkoani Morogoro baada ya
kutembelea viwanda viwili ambavyo ni Philip Morris Tanzania (PMT) cha
kutengeneza sigara aina ya Marlboro pamoja na kiwanda cha mafuta ya kula
cha Moproco.
“Wale wote waliochukua viwanda vya Morogoro vifanye kazi, hatutaki
kusikia kiwanda hakifanyi kazi na uzalishaji wake kwa kutumia malighafi
ya ndani ili kuwezesha kuteneza ajira za moja kwa moja na nyingine
zisizo za moja kwa moja kupitia uzalishaji wa mazao yanayotumika kama
malighafi ya viwanda,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema serikali zote zilizopita zimekuwa na mikakati ya ujenzi wa
viwanda tangu awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa kuweka dira ya
maendeleo ya viwanda.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inahakikisha Tanzania inakuwa na
mazingira mazuri ya kibiashara na kuendelea kujenga mazingira ya kukuza
uchumi unaoendelea kukua. “Tanzania imepanga kuona mazingira ya uchumi
yanaboreka ili kuvutia wawekezaji na ili kufikia lengo hili ni lazima
serikali ya mkoa isimamie masuala ya uwekezaji na kulinda mafanikio yake
na hii ni pamoja na ngazi za wilaya,” alieleza Waziri Mkuu.
Pamoja na hayo, aliwataka Watanzania wenye kubahatika kupata ajira za
viwandani, kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuwa waadilifu kwa
kuacha wizi na hujuma mbalimbali ili kuwatia moyo wawekezaji kupanua
ajira zaidi kutokana na faida watakayoipata ya uwekezaji wao.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage alisema moja ya jukumu alilonalo ni kuhakikisha viwanda vyote
vya umma vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji vinafanya kazi ikiwa na
kuvifufua upya na kuanzisha viwanda vipya.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment