Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
RAIS John Magufuli amefuta umiliki wa mashambapori 14 yaliyopo mkoani
Morogoro yasiyoendelezwa yenye jumla ya ukubwa wa ekari 15,567.6
yakiwamo ya mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Jeetu Patel na
la Esther Sumaye ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye.
Aidha, serikali imesema haifuti umiliki wa mashamba kwa kuonea mtu,
itikadi zake za kisiasa, dini, rangi ama kabila, bali inazingatia
misingi ya kisheria iliyowekwa kwa wale wote wasioyandeleza kwa miaka
mingi ikiwamo kushindwa kulipia kodi ya ardhi iliyowekwa kwa mujibu wa
sheria na kanuni za ardhi zilizopo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alisema hayo jana katika kikao maalumu cha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Dk
Stephen Kebwe pamoja za wilaya ya Kilosa na Mvomero, kilichohusu
kutolewa kwa taarifa juu ya kufutwa kwa mashamba pori 14 ya mkoa huo na
Rais Magufuli.
Lukuvi aliwaambia wajumbe hao kuwa Rais amefuta umiliki wa mashamba
pori 14 yaliyopo mkoani humo yasiyoendelezwa yenye jumla ya ukubwa wa
ekari 15,567.6, baada ya uongozi wa wilaya za Morogoro, Kilombero,
Kilosa na Mvomero, kuwasilisha mapendekezo kwake kuomba kufutwa kwa
mashamba pori hayo na kuyawasilisha kwa Rais.
Alieleza kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, wananchi
wa Mkoa wa Morogoro walitoa kilio chao juu ya ukosefu wa ardhi ya
kilimo kutokana na mashamba mengi kuhodhiwa na watu wachache na
kushindwa kuyandeleza na wengine kuwakodishia.
Alisema baada ya Rais kuingia madarakani, alifanyia kazi mapendekeo
yaliyowasilishwa na waziri baada ya kupokea kutoka viongozi wa
halmashauri na mkoa huo kuhusu kufutiwa hatimiliki zao.
Alisema Rais ametekeleza jambo hilo kwa kuyafuta mashamba pori 14
yakiwemo matano ya Noble Agricultural Enterprises Ltd yaliyopo katika
Kijiji cha Mvumi, Wilaya ya Kilosa lenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,661
ambayo ni ya mfanyabiashara maarufu Jeetu Patel pamoja na la mkewe
Sumaye, Esther.
“Rais anapofuta hatimiliki ya mashambapori, anazingatia utaratibu wa
kisheria bila kumwonea mtu kulingana na dini yake, rangi yake, kabila
ama itikadi ya chama,” alisema Lukuvi na kuongeza mashamba mengi
yanafutwa kwa kusababishwa na wamiliki wenyewe kwa kushindwa kufuata
masharti ya ardhi yakiwemo kukosa kulipa kodi ya serikali kipindi kirefu
na kutoyandeleza cha asilimia zilizotajwa na kisheria na kubakia ni
mapori.
Lukuvi aliyataja mashambapori yaliyofutwa umiliki wake yakiwemo
manane kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa likiwemo la Jitu na mawili
kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, miongoni mwa hayo ni la Esther
Sumaye lenye namba 21919 likiwa na ukubwa wa ekari 473.
Mashambapori mengine yaliyofutiwa umiliki wake ni pamoja na mashamba
manne ya Noble Agricultural Enterprises Ltd yaliyopo katika Kijiji cha
Mvumi Wilaya ya Kilosa lenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,661.
Lukuvi alitaja mashambapori mengine mawili tofauti yaliyokuwa
yakimilikiwa na Shanta Estate Co Ltd yaliyopo Msowero pia wilayani
Kilosa yenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,200 na shambapori jingine ni
lililokuwa linamilikiwa na New Msowero Farms Ltd yenye ukubwa wa ekari
1,769.
Mashambapori mengine ni la Darbrew Limited lenye ukubwa wa hekta
386.7 lililopo Msowero, shamba lililokuwa linamilikiwa na James Longido,
Saidi Longido, Lengai Lupejo, Sefu Longido na Maboli Sangati yenye
ukubwa wa hekta 224. 62 yakiwa katika Kijiji cha Wami Luhindo wilayani
Mvomero.
Waziri Lukuvi pia alitaja mashamba mengine yasiyoendelezwa
yaliyofutiwa hatimiliki na Rais ni Nguru ya Ndege Morogoro lililokuwa
likimilikiwa na Guard Kiangi lenye ukubwa wa ekari 100 pamoja na shamba
lenye hekta 192.12 lililopo eneo la Wami Luhindo, Mvomero ambalo
lilikuwa likimilikiwa na Ndeshukurwa Sumari.
Mashambapori mengine yaliyofutwa umiliki wake ni Sangasanga Morogoro
lililokuwa linamilikiwa na Leila Omari lenye ukubwa wa ekari 326 na
jingine ni la Usafirishaji Mikoani Union Ltd lenye ukubwa wa ekari 6,010
lililipo katika Kijiji cha Ruipa Wilaya ya Kilombero.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe alisema mkoa huo
una mashambapori 223 na kati ya hayo, 198 yapo katika Wilaya ya Kilosa
na kwamba kazi ya kuainisha inaendelea kufanywa na timu ya wataalamu wa
mkoa huo ili yawasilishwe kwa waziri mwenye dhamana.
Hata hivyo, alitoa onyo kwa wananchi kuacha kuyavamia mshamba pori
yaliyofutiwa umiliki wake na Rais na badala yake wasubiri utaratibu
utakowekwa na serikali ya mkoa na halmashauri za wilaya husika kwa
mujibu wa sheria ili kuweka matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya watu
wa nchini.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment