Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wanawake
na vijana wanaopewa mikopo na Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa
Ifakara mkoani Morogoro wamekumbushwa kupeleka marejesho kwa wakati ili
kuwapa fursa na wananchi wengine kupata mikopo hiyo.
Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Christopher Msimbe ameyasema hayo hivi
karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
kuhusu nafasi ya vijana walemavu waliomaliza mafunzo kupitia Mradi wa
Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan
International.
Msimbe
amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali, Halmashauri
inatambua nafasi ya vijana katika jamii hasa vijana wenye ulemavu na
ndio sababu wanawakumbuka katika fursa nyingi zinazokuja katika
Halmashauri hiyo kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Katika
Halmashauri yetu tumebahatika kupata mradi wa YEE unaowashirikisha hata
vijana wenye ulemavu, mradi huo unalenga kuwapatia mafunzo ya ufundi
vijana ili waweze kujitegemea hivyo sisi kama Serikali tumetoa jumla ya
shilingi 4,000,000 kwa vikundi viwili vya vijana wenye ulemavu ili
waweze kuinua shughuli zao,”alisema Msimbe.
Amefafanua
kuwa Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya
kuwapatia mikopo vijana na wanawake ili kuwasaidia kujikwamua kimaisha
kwa kuendelezea biashara zao lakini asilimia kubwa wamekuwa hawapeleki
marejesho kwa wakati na kusababisha Halmashauri kushindwa kutoa mikopo
kwa watu wengine.
Nae,
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiungwile “A” iliyopo wilayani Kilombero Mkoa wa
Morogoro, Emmanuel Sama amesema mradi huo umewasaidia vijana wengi kwa
sababu kabla ya mradi huo vijana walikuwa wakizurura mitaani bila kazi
yoyote pia vijana walemavu walikuwa wakikaa ndani bila kujua hatima yao.
“Mtaani
kwangu nina vijana watano waliopewa mafunzo na shirika hili ambao
wamefanikiwa kuunda kikundi chao kijulikanacho kama ‘Baraka Farmers
Group’ ambacho kinatumia elimu waliyoipata pamoja na mkopo wa shilingi
1,500,000 kutoka katika Halmashauri yetu kujiendeleza kiuchumi,
nawashkuru vijana hawa kwani wanatumia vizuri fursa waliyopewa na
kurejesha fedha walizokopeshwa kwa wakati,”alisema Sama.
Sama
ametoa rai kwa wananchi wanaopewa mikopo na Serikali hasa wananchi
wasio na ulemavu ambao wanaweza kufanya kazi kwa uhakika kurejesha fedha
za mikopo kwa wakati ili Halmashauri iweze kuendelea kuwasaidia
wananchi wengine na watakaokaidi watachukuliwa hatua stahiki ili
warudishe fedha hizo.
Mradi
huo wa miaka mitatu umeanza mwaka 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa
ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na
Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International
chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
0 comments:
Post a Comment