Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, James Ihunyo amewataka vijana
wenye ulemavu kuchangamkia fursa zitolewazo na Serikali pamoja na wadau
mbalimbali ili ziwasaidie kuboresha maisha yao.
Mkuu
huyo wa Wilaya ya Kilombero ameyasema hayo leo wakati alipokuwa
akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya ushiriki wa walemavu
katika Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na shirika
la Plan International.
Mhe.
Ihunyo amesema asilimia kubwa ya vijana wenye ulemavu wamekosa nafasi
ya kupata elimu na wengine wameishia njiani hivyo ili kuwafanya wawe
sawa na vijana wengine Halmashauri ina wajibu wa kuwapatia mafunzo ya
ufundi ili waweze kujiajiri na kujipatia vipato vitakavyowawezesha
kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa.
“Katika
maeneo mbalimbali nchini walemavu wamekuwa wakitengwa na wengine
kufichwa ndani ikiaminika kuwa hawawezi kufanya shughuli yoyote, kwa
kupitia mradi wa YEE unaoratibiwa na shirika la Plan International
ninawaomba vijana walemavu kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa
hiyo,”alisema Mhe. Ihunyo.
Ameongeza
kuwa tangu mwaka 2015 mradi ulivyoanzishwa jumla ya vijana 1376
wameshapatiwa mafunzo chini ya mradi huo lakini vijana wenye ulemavu ni
13 tu ambayo ni sawa na asilimia 3 kati ya asilimia kumi iliyopangwa
katika mradi huo hivyo vijana walemavu wanatakiwa kujitokeza kwa wingi
kwani mradi huo una manufaa katika maisha yao.
Aidha,
Mhe. Ihunyo ametoa wito kwa watendaji wa Serikali za Vijiji, Kata na
Vitongoji kujitahidi kuwaibua vijana walemavu ili waweze kupatiwa
mafunzo yatakayowasaidia kuimarisha maisha yao pamoja na Taifa kiujumla.
Amefafanua
kuwa Serikali inashirikiana na Shirika hilo katika kutoa maeneo ya
kufundishia pamoja na kutoa mikopo inayotumika kama mitaji ya kuanzishia
shughuli mbalimbali kwa vijana wanaohitimu mafunzo hayo.
Kwa
upande wake mzazi wa kijana mwenye ulemavu, Menhad Limota amelishkuru
shirika hilo kwa kuweza kuwapatia vijana hao mafunzo ya ufundi pamoja na
ushauri wa kitaalamu ambao umewawezesha kufanya shughuli zao
zinazowasaidia kupata fedha za kujikimu.
“Miaka
ya nyuma kabla mwanangu hajapatiwa mafunzo alikuwa akinitegemea mimi
kwa kila kitu lakini baada ya mafunzo hayo ameweza kujiunga na walemavu
wenzie na kuanzisha shughuli mbalimbali ambazo kwa namna moja au
nyingine zinamsaidia yeye pamoja na sisi wazazi wake,”alisema Limota.
Mradi
huo wa miaka mitatu 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa
mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya
Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya
ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
0 comments:
Post a Comment