Na Ally Daud
MAELEZO
MOROGORO.
WIZARA
ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia
,Wazee na Watoto kupitia kitengo cha Magonjwa yasioambukiza (NCD) chini ya
Kurugenzi ya Tiba inaendesha mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa
watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya.
Akifungua
mafunzo hayo leo jijini Morogoro Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt.
Margaret Mhando amesema kuwa wameamua kuanzisha mpango huo ili kuwapa nguvu na
uwezo watoa huduma kwa ajili ya kupambana na magonjwa hayo.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana
duniani na haswa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hivyo hatuna budi kuongeza
juhudi za kupambana nayo” alisema Dkt. Mhando
Aidha Dkt. Mhando amesema kuwa pamoja na juhudi
zinazofanywa na Wizara katika kupambana na magonjwa hayo kila mkoa na wilaya
lazima ziangalie uwezekano wa kuifanya NCD kuwa kipaumbele katika mipango yao
ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mhando amesema kuwa viashiria
vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza imeonyesha kuongezeka kwa hali ya juu
ambapo idadi ya watu wanaovuta sigara ni
asilimia 15.9 wanaokunywa pombe ni asilimia 29.3, wenye uzito uliopita kiasi 34.7,
shinikizo la damu ni asilimia 25.9 na wagonjwa wa kisukari ni asilimia 9.1.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa
Magonjwa yasioambukiza Dkt. Sarah Maongezi amesema kuwa wanatakiwa kupunguza
moja ya tatu ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kukinga,
kutibu na kuzingatia afya ya akili Kufikia mwaka 2030.
Aidha Dkt. Maongezi amesema kuwa wanatarajia waganga wa ngazi za mikoa na
wilaya kufanya kazi kwa nguvu na kwa ukaribu zaidi na kitengo cha magonjwa
yasiyo ya kuambukiza cha Wizara ili huduma hizi ziwafikie watu wote hadi ngazi
ya jamii.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika jijini
Morogoro yanalenga kuwafundisha madaktari na watoa huduma kuhusu kupambana na
ya magonjwa yasioambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la
damu, kansa, ajali za barabarani na
uzito kupita kiasi.
0 comments:
Post a Comment