Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mpango
Bora wa Matumizi ya Ardhi utakaobainisha mipaka kati ya Kijiji kimoja
na kingine pamoja na maeneo husika ya makazi unatarajiwa kunufaisha
jumla ya Vijiji 30 nchini.
Hayo
yamesemwa hivi karibuni na Meneja Miradi wa Shirika la PELUM –
Tanzania, Rehema Fidelis wakati wa mafunzo kwa wajumbe wa Halmashauri za
Vijiji, Mabaraza ya Ardhi, Kamati za Maamuzi pamoja na wananchi
yaliyolenga kuwaongezea maarifa na uelewa ili kuimarisha haki za ardhi
kwa wakulima wadogo chini ya Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika
Kusimamia Sekta ya Kilimo.
Bi.
Rehema alisema kuwa shirika hilo limeamua kushirikiana na Serikali
katika kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyokithiri nchini inapata
suluhisho kwani wamebaini kuwa vijiji vingi havijafanyiwa mpango wa
matumizi bora ya ardhi jambo linalochochea kuwepo kwa kutokuelewana
baina ya kijiji kimoja na kingine na hivyo kuibua migogoro ya ardhi.
“Vijiji
vitakavyonufaika ni vya Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Iringa ambapo
mpango huu utasaidia kubainisha maeneo ya shughuli za kijamii, malisho
na kilimo kama njia mojawapo ya kupunguza migogoro ya ardhi baina ya
wakulima, wafugaji na wawekezaji,” alisema Bi. Rehema.
Amefafanua
kuwa mpango huo unatarajia kunufaisha wananchi 10,000 toka vijiji 30
vya wilaya za Morogoro mjini na Mvomero, Bahi na Kongwa (Dodoma) pamoja
na Kilolo na Mufindi (Iringa) ambapo kila wilaya itawakilishwa na vijiji
vitano.
Akibainisha
matokea ya awali ya mradi huo, Afisa Mipango Miji wa Wilaya ya Kongwa,
Meshack Sylvester alisema kuwa mafunzo waliyopewa wanakijiji hao
yamewafanya kuwa na uelewa hivyo kukubali kukaa pamoja na uongozi wa
vijiji vyao kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya amani.
Mbali
na kufanikiwa kutatua migogoro hiyo, Sylvester alisema kwa sasa jamii
imekuwa na uelewa juu wa wanawake kuweza kupata fursa mbalimbali
zinazotokana na uwepo wa ardhi kama ilivyo kwa wanaume.
“Awali
wanawake walikuwa wakinyanyasika kutokana na mila na desturi, hivyo
kukosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kumiliki, kuuza na kurithi
ardhi lakini kwa sasa jamii imepata uelewa na wapo wanawake ambao tayari
majina yao yameingizwa kwenye idadi ya watu ambao watapata hatimiliki
za kimila za mashamba yao wakati zoezi likiendelea” alisema
Sylvester.
Ameongeza
mafanikio mengine ya mradi huo kuwa ni kuweza kuundwa kwa kamati 26 za
kushughulikia migogoro midogomidogo ya mipaka na haki za wanawake
walemavu na wajane kwani mwanzo kabla ya mradi kulikuwa na kamati tano
pekee.
Naye
mkulima kutoka kijiji cha Lenjulu wilayani Kongwa, Yohana Sulutya
amelipongeza zoezi hilo kwani litatatua migogoro ya ardhi katika vijiji
vyao pia mafunzo waliyopatiwa yamewasaidia kufahamu sheria na kanuni
mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi ikiwemo kujua kuwa wanakijiji
ndio wenye mamlaka ya mwisho juu ya ardhi ya kijiji pamoja na kufahamu
kuwa viongozi wa kijiji na kamati husika za masuala ya ardhi hawana
mamlaka ya kuuza ardhi ya kijiji pasipo maridhiano na wanakijiji kupitia
mkutano mkuu wa kijiji.
Naye
Samwel Saning’o mfugaji kutoka Kijiji cha Kibaoni wilayani Mvomero,
alikiri kuwepo kwa migogoro ya ardhi mara kwa mara katika wilaya ya
Mvomero baina ya wakulima na wafugaji, na kubainisha kuwa migogoro mingi
inachangiwa na wanavijiji kutokufahamu mipaka ya vijiji yao ikiwa ni
pamoja na vijiji kutokufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na
kuchangia kufuata malisho, majosho ama maji ya mifugo maeneo ya mbali.
Kwa
upande wake Fransisca Mtizi kutoka kijiji cha Kongogo Wilaya ya Bahi
aliiomba Serikali kumalizia kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi
kwenye vijiji vilivyobaki pamoja na kugawa hatimiliki za kimila kwenye
mashamba ya wakulima wengine ambao vijiji vyao havikuingia kwenye mradi
huu ili kuleta usawa baina yao.
0 comments:
Post a Comment