Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Wataalamu
wa kilimo wamewataka wakulima mkoani Morogoro kutumia pembejeo za asili
ili kuepuka kemikali zenye sumu zinazotokana na pembejeo za viwandani
ambazo zinaathiri usalama wa chakula.
Rai
hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini Morogoro katika mafunzo ya siku moja
yaliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania wakishirikiana na Shirika
la TOAM kupitia Mradi wa Masuala ya Kilimo Unaozingatia Utunzaji wa
Mazingira.
Akifungua
mafunzo hayo, Mratibu wa Shirika linalohamasisha utunzaji wa bionuwai
ya kilimo Tanzania (TABIO), Abdallah Ramadhani amesema kuwa lengo
la mafunzo hayo ni kuweza kutoa elimu juu ya umuhimu na matumizi sahihi
ya pembejeo za asili kwa ajili ya kukuza na kuendeleza kilimo hai
nchini hasa kwa kuangalia njia zinazotumika kutengeza mbolea na madawa
ya asili ili kuhakikisha wakulima nchini wanaachana na matumizi ya
viuatilifu vya viwandani ambavyo vina kemikali.
“Viuatilifu
vyenye kemikali za kuua wadudu waharibifu zenye thamani ya Dola za
Kimarekani Bilioni 30 humwagwa kwa makusudi katika mazingira ya dunia
kila mwaka, sehemu kubwa ya viuatilifu hivyo ni vile vyenye sumu kali
ambazo zina athari za moja kwa moja kwa afya ya binadamu, wanyama pori
pamoja na vyanzo vya chakula ndio maana tunawashauri wakulima kuacha
kutumia pembejeo za aina hiyo”,alisema Ramadhani.
Akibainisha
baadhi ya madhara yatokanayo na viutalifu hivyo toka viwandani,
Ramadhani amesema kuwa pamoja na kuathiri afya na usalama wa viumbe hai,
viuatilifu hivyo vinatumiwa bila ya kuwa na vifaa kinga pia huchafua
mzingira na hata kuua viumbe wengine wasiokusudiwa.
Ameongeza
kuwa, baadhi ya viuatilifu hivyo vina athari za muda mrefu kwa binadamu
ikiwemo matatizo ya uzazi, dosari za kuzaliwa, kuvuruga mfumo wa homoni
na kuharibu mfumo wa kinga.
Kwa
upande wake Meneja wa Viwango na Ubora toka Kampuni ya Guavay
inayotengeza mbolea aina ya HAKIKA Organic Fertilizer, Latifa Mafumbi
amewasihi wakulima kuendelea kutumia pembejeo za asili kwa kuwa hazina
madhara kuanzia kwa mtengenezaji, ardhi, mimea, viumbe, wadudu
wanaorutubisha ardhi pamoja na mlaji.
Amesema
kuwa kama mtaalamu, kwa sasa anaendelea kufanya uchunguzi kwenye zao la
nyanya ili kubaini tofauti iliyopo kwenye zao hilo kama atatumia mbolea ya
kiwandani yenye kemikali na mbolea iliyotengenezwa kiasili kwani tafiti
nyingi za awali zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea za asili hutoa
mazao bora.
Naye
mkulima mshiriki, Pius Paulini amebainisha kuwa kilimo hai
kinachotokana na matumizi ya pembejeo za asili (mbolea na madawa)
kimekuwa kikiongeza rutuba kwenye ardhi hivyo kuwasaidia wakulima kulima
kwenye eneo moja kwa kipindi kirefu pasipo kuhamahama.
Amefafanua
kuwa mimea hustahimili mabadiliko ya tabianchi tofauti na viuatilifu
vya viwandani vilivyojaa kemikali yenye sumu na kuchangia kwa asilimia
kubwa kufifisha ubora wa ardhi na hata kuua wadudu ambao wanasaidia
kurutubisha mimea shambani.
PELUM
ni shirika linalohamasisha utunzaji na matumizi bora ya ardhi kwa ajili
ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuepuka athari kwenye
kilimo na shirika la TOAM ni shirika linalohamasisha Kilimo Hai Tanzania.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment