May Simba na Lorietha Lawrence-MAELEZO
Ardhi ni kiwanda mama kwa maisha ya Watanzania na pia ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi nchini.
Maendeleo
ya sekta ya ardhi nchini yamekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
migogoro ya muda mrefu baina ya jamii na wawekezaji, umiliki usio rasmi
pamoja na ujenzi wa makazi holela.
Kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya Ardhi nchini kumesababisha Serikali kuboresha Sera ya Ardhi ya mwaka 1995.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwa kero kwa wananchi walio wengi.
Taarifa ya Wizara hiyo inasema jumla ya migogoro 1,378 iliripotiwa Serikalini hadi kufikia Oktoba 2016, ambapo migogoro 690 ilitatuliwa kiutawala.
Aidha jumla ya mashauri 3,968 yalitolewa maamuzi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
Wizara
hiyo pia imefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu uliodumu kwa Zaidi
ya miaka 15 katika maeneo ya Chasimba iliyopo katika eneo la Wazo Hill
Jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya hekari 200 ya ardhi zilizokuwa na
mgogoro baina ya wananchi na Uongozi wa kiwanda cha saruji cha Twiga
umetatuliwa.
Migogoro mingine iliyotatuliwa kwa kipindi hicho ni pamoja na ule wa shamba la Kapunga Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited mgogoro huu uliodumu kwa miaka 10, ambapo hekta 1,780 zimerejeshwa kwa wananchi.
Katika
upande wa uboreshaji wa huduma kwa umma, Wizara imeimarisha utendaji
kazi katika kituo cha huduma kwa wateja kwa kuongeza idadi ya watumishi,
vifaa na aina ya huduma za ardhi zinazotolewa.
Kutokana
na maboresho hayo, idadi ya siku za kuandaa hati imepungua kutoka zaidi
ya siku tisini (90) hadi kufikia chini ya siku sitini (60).
Aidha Wizara ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, imeunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mapya 47.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekosti na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani, na Haki za Binadamu, Askofu William Mwamalanga alipongeza mafanikio yaliyopo sasa katika sekta ya ardhi, hatua inayotokana na Uongozi imara wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Askofu
Mwamalanga anasema utafiti uliofanywa na kamati yake umebaini kuwa
asilimia 91 ya migogoro ya ardhi hapa nchini imepungua.
“Kamati
ilifanya tafiti katika ngazi za Mikoa , Wilaya na Kata zote na kubaini
kuwa migogoro ya ardhi nchini imepungua sana ukilinganisha na hali
ilivyokuwa hapo awali”, alisema Askofu Mwamalanga.
Askofu Mwamalanga aliongeza kuwa mbali na kutatuliwa kwa migogoro ya ardhi pia wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi wamekuwa wakifanya kazi kwa maadili na uadilifu mkubwa.
Aliongeza
kuwa katika kipindi cha nyuma sekta ya ardhi ilikuwa ikiongozwa kwa
rushwa lakini katika uongozi wa Rais,Dkt.Magufuli kumekuwepo na hofu ya
rushwa na uwajibikaji huku kila mtu akiwa mlinzi wa mwenzake.
Kwa
mujibu wa Askofu Mwamalanga utafiti huo pia umebaini kuwa wafanyakazi
wa sekta ya Ardhi katika halmashauri wamekuwa wakitoa ushirikiano wa
hali ya juu katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa muda na wakati
uliopangwa.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment