Mwalimu wa serikali agundulika kulipwa mishahara miwili
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe
MWALIMU wa Shule ya Sekondari Masagati inayomilikiwa na serikali
katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro, Justian
Julias amegundulika kuajiriwa mara mbili, ikiwamo katika shule nyingine
binafsi na kuendelea kulipwa mishahara miwili kwa nyakati tofauti.
Mwalimu huyo amebainika na wajumbe wa timu ya mkoa ya uhakiki wa kina
kwa watumishi hewa iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen
Kebwe.
Julias ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Masagati ya serikali na
katika uhakiki wa kina aligundulika akiwa na ajira nyingine katika shule
binafsi ya Mbingu wilayani Kilombero.
Timu hiyo ilipita katika halmashauri zote za mkoa huo kufanya uhakiki
wa kina kuanzia Mei 12 hadi Julai 12, mwaka huu na jumla ya watumishi
batili 315 waliobainika katika uchunguzi huo na Halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa ikiongoza kwa watumishi hewa 98 ikifuatiwa na Mji wa Ifakara kwa
watumishi hewa 48.
Mkuu wa mkoa huyo alisema hayo kwa waandishi wa habari jana kwenye
kikao cha kujadili utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan kuhusu kutenga maeneo ya malisho na kutumia fursa hiyo
kutoa taarifa ya watumishi hewa na kukamilishwa kwa zoezi la uhakiki wa
kina katika halmashauri zote nane za mkoa huo.
“Mwalimu huyo analipwa mishahara miwili na waajiri wawili
tofauti...nimeagiza hatua za kisheria zichukuliwe kwa mkuu wa shule na
mwalimu mwenyewe na taarifa zake ziwasilishwe kwangu mara moja,”
alisisitiza Dk Kebwe.
Dk Kebwe aliunda timu ya watu saba ya uhakiki wa kina watumishi hewa
kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na Sekratarieti ya Mkoa iliyoongozwa
na Mwenyekiti Marieta Njovu, ambayo imebaini fedha zilizolipwa kutokana
na watumishi hao hewa ni Sh 2,213,997,780.78. Kati ya hizo,
zilizokwisha rejeshwa serikalini ni Sh 42,762,779.98.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment