Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei
POLISI mkoani hapa inamshikilia mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina ya
Zakaria Benjamin Migomba (35) mkazi wa Tungi, Manispaa ya Morogoro, kwa
tuhuma za kuingia isivyo halali katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Morogoro na kujifanya kuwa ni daktari.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huu, Ulrich Matei alisema tukio hilo
lilitokea Julai 10, mwaka huu, saa 10: 00 alfajiri ambako mtuhumiwa huyo
aliingia katika hospitali hiyo kwa nia ya kutenda kosa.
Alisema mtuhumiwa huyo alitembelea wodi mbalimbali ikiwemo namba moja
na namba tisa na alipofika wodi namba saba, alienda moja kwa moja eneo
la chumba cha kubadilisha nguo na kuchukua koti la daktari na kulivaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, baada ya kuchukua koti na kulivaa
alikwenda moja kwa moja wodi ya wagonjwa mahututi ambapo alipofika
wodini hapo muuguzi wa zamu alimshtukia na kuiarifu Polisi juu ya mtu
huyo.
Kamanda alisema askari walipopata taarifa hiyo walifika mara moja
hospitalini hapo na kumkuta mtuhumiwa huyo na alipohojiwa alidai kuwa
yeye ni daktari mgeni alikuwa akitembelea wagonjwa ili kukagua na kuona
kama wanapatiwa huduma ipasavyo.
“Tayari alikuwa ametembelea wodi kadhaa ikiwemo namba moja, tisa na
saba ambapo alichukua koti la daktari na kulivaa akijifanya kuwa yeye ni
daktari mgeni hivyo anakagua wagonjwa kuona kama wanapatiwa huduma
ipasavyo,” alisema Kamanda Matei.
Hivyo alisema baada ya kukamatwa alipohojiwa na kufanyika uchunguzi
wa awali ilibainika kuwa yeye si daktari wala mfanyakazi wa hospitali
hiyo na kwa sasa anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi kutokana na kauli zake
kuwa yeye ni askari mpelelezi na pia kuona iwapo akili yake iko sawa.
Kwa upande wake, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kuwa ni Zakaria
Benjamin Migomba kutoka Gairo na kwamba elimu yake ni darasa la saba.
Inaelezwa kuwa wakati huo huo alitoa maelezo yanayojichanganya kuwa
ni askari wa jeshi la kujitegemea aliyefika hospitalini hapo kufanya
kazi ya Rais, jambo lililowapa wasiwasi juu ya utimamu wa akili yake.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment