Na Benedict Liwenga, MAELEZO
Halmashauri ya Wilaya
ya Morogoro imeviwezesha Vikundi 39 vya Wanawake pamoja na Vijana vyenye
wanachama 295 kupatiwa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 23.8 kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake.
Taarifa hiyo
imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo
(Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe.
Tebweta Omary lililotaka kujua mpango wa Serikali wa kuzibana na
kuziamuru Hallmashauri zote ikiwemo ya Morogoro Vijijini kutenga
asilimia 5 ya fedha za mapato ya ndani kwa Vijana na asilimia 5 kwa
ajili ya akina mama.
Mhe. Jafo
amesema kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2015/16, Serikali imetenga
shilingi milioni 175 kwa ajili ya wanawake na vijana kutokana na mapato
ya ndani.
Amefafanua
kuwa, mkakati wa sasa wa Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili
kujenga uwezo wa kutenga fedha zaidi ambapo katika bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2016/17 sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila
Halmashauri lilikuwa ni kuonyesha asilimia 10 zilizotengwa kwa ajili ya
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake kutokana na mapato ya ndani.
"Halmashauri
zote zimeagizwa kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa kwenye vikundi
husika ikijumuisha walemavu na kusimamia marejesho yake ili vikundi
vingine viweze kunufaika.
Kwa upande
mwingine, Mhe. Jafo amejibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Kanyasu
Costantine John ambaye alitaka kujua kwanini Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Nyankimbo imabaki kuwa shule ya Kutwa wakati mazingira yake
yanafaa kuwa sekondari ya Bweni ambapo alijibu kuwa shule hiyo
ilijengwa chini ya Mradi wa Geita Giold Mining na kupata usajili wa Na.
S.1942 mwaka 2006 ikiwa ni shule ya kutwa kwa kidato cha Kwanza hadi cha
Nne.
Aidha,
amesema kuwa mwaka 2012 shule hiyo iliongezewa kidato cha Tano na Sita
hali iliyoifanya shule hiyo kuwa imesajiliwa ya kutwa kwa kidato cha
kwanza hadi cha nne na Bweni kwa kidato cha Tano na Sita.
"Taratibu zilizotumika ili kuisajili shule kuwa ya bweni
ni Halmashauri yenyewe kuwasilisha maombi Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi ili kupata kibali", alisema Mhe. Jafo.
Aliongeza
kuwa, kabla ya kupata usajili, Kamishna wa Elimu atatuma Timu ya
Wataalam katika shule husika kwa ajili ya kuhakiki uwepo wa miundombinu
inayohitajika ilio shule iweze kusajiliwa kuwa ya bweni.
0 comments:
Post a Comment