WAKATI Serikali ikielekeza nguvu zake katika mapinduzi ya uchumi
kupitia viwanda, mkoa wa Morogoro umejiweka katika nafasi nzuri ya
kunufaika kutokana na kuongezeka kwa kasi ya miradi ya umeme.
Tayari Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) liko kwenye hatua za mwisho
za kumalizia miradi mikubwa ya umeme, ukiwamo mradi wa umeme mijini na
ule unaofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambapo zaidi ya watu
11,300 wanatarajiwa kunufaika.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mhandisi wa umeme wa Tanesco mkoani
Morogoro, anayeshughulikia masuala ya ujenzi, David Chisot alisema
kupitia miradi hiyo, wateja wakubwa na wadogo watafikiwa na nishati ya
umeme katika maeneo ambayo awali hayakuwa na umeme kabisa.
Alisema wananchi hao watapata fursa ya kuanzisha viwanda vidogo na
vikubwa katika maeneo yenye fursa ya malighafi za uzalishaji, wananchi
kujiajiri na kuongeza ajira kwa wengine na kufanya maendeleo mengine
yanayohitaji nishati ya umeme katika maeneo yao.
Chisot alifafanua kuwa miradi inayofadhiliwa na Rea itahusisha wilaya
nne za mkoa wa Morogoro ikiwemo Morogoro katika vijiji 27, Mvomero
vijiji 35, Kilombero vijiji vinne na Ulanga vijiji vitano ambapo tayari
wateja 5,562 wa mradi wa Rea wameanza kunufaika na mpango huo wakiwamo
wateja wadogo 5,457 na wakubwa 205.
Alisema, “Kuna miradi mipya 69 inayogharimu Sh bilioni nane
inayotekelezwa, katika hiyo miradi 18 imekamilika, 28 wakandarasi wapo
maeneo ya kazi wakiendelea na ujenzi na 23 haijaanza huku miradi 38
ikiwa ni endelevu na kati yake 10 tayari imekamilika na 12
haijakamilika, lakini wakandarasi wanaendelea na umaliziaji”.
Alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo, changamoto mbalimbali
zimeendelea kujitokeza, ikiwamo watu kudai fidia pale wanapokwenda
kuweka nguzo za umeme katika nyumba au wanapopitisha nyaya za umeme
katika maeneo ya makazi na wengine kufanya uharibifu wa kukata miti na
kuwafanya kukosa umeme wakisingizia Tanesco ndio waliokata umeme huo.
“Naomba niweke wazi kuwa umeme wa Rea haina fidia, kuna maeneo
tulishapita na kuweka njia, lakini ukirudi kwenye kazi unakuta nyumba
zimezuia, hii inatuathiri sana, lakini inawaathiri wananchi ambao ndio
wafaidika wakubwa wa umeme,” alisisitiza Chisot.
Aidha, amewasihi wananchi kuacha kuwatumia vishoka au njia
zisizostahili hasa pale wanapohitaji huduma ya umeme na kuwataka wafuate
njia sahihi ikiwemo kufika ofisi za Tanesco kwa maelekezo juu ya kupata
huduma za shirika.
Chisot aliwashauri wateja ambao tayari wamefikiwa na huduma hiyo
waisaidie Tanesco kwa kufunga nyaya katika nyumba zao ili iwe rahisi
kufungiwa umeme, lakini akawaonya wateja kutojiunganishia umeme kutoka
kwa mafundi wasio rasmi ambao hawatambuliki na shirika hilo.
Kwa upande wao, wananchi wa Morogoro wameelezea matumaini yao juu ya
mpango huo wa Tanesco, ambapo baadhi yao Issaya Kennedy, Lucas Simon na
Marietha Kitaly walisema hatua hiyo ni nzuri na itasaidia kuharakisha
maendeleo.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment