Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe ameziagiza halmashauri zote
mkoani kwake kununua picha za anga ili mpango wa upimaji ardhi
unaofanywa na mradi wa kuwezesha umilikishaji ardhi (LTSP) mkoani hapa
uweze kuwa wa kisasa zaidi.
Akifungua mkutano wa mawasilisho ya mpango wa matumizi ya ardhi wa
Wilaya ya Kilombero, Dk Kebwe alisema kwamba ili mradi wa LTSP uweze
kuwa wa manufaa, ni lazima halmashauri zinunue picha hizo. Mradi huo
unatekelezwa katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.
“Gharama za satellite image (picha za anga) ni kati ya Sh milioni 80
na 100, naziagiza halmashauri zote kuhakikisha kwa mwaka huu zinanunua
satellite image ili tuweze kupima ardhi yetu kisasa zaidi kuliko
utaratibu huu tunaotumia sasa ni wa kizamani zaidi,” alisema Dk Kebwe.
Dk Kebwe alisema picha hizo zitasaidia halmashauri kutambua ardhi na
majengo yaliyopo katika maeneo yao na kutoza kodi. Alisema halmashauri
ziache visingizio vya kutokuwa na pesa za kununua picha hizo hadi
kusubiri fedha za wahisani wa maendeleo.
Katika hotuba yake, mkuu huyo wa mkoa alisema upimaji huo wa ardhi
utasaidia kuondoa migogoro ya ardhi katika mkoa wake na akaonya kuwa
wale wote ambao wana mashamba makubwa katika mkoa wake na
hayajaendelezwa yatachukuliwa na kugawiwa kwa watu ambao wana matatizo
ya ardhi.
Aliwahakikishia kuwa barabara ya kutoka Kidatu kwenda Ifakara mjini
itajengwa kwa kiwango cha lami kwani tayari Umoja wa Ulaya umeshatoa
fedha za kujenga barabara hiyo. Alisema upimaji wa ardhi ukikamilika na
barabara ikajengwa wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi zitapiga hatua
kubwa kwa maendeleo.
Kiongozi wa timu ya urasimishaji ya ardhi wa LTSP Swagile Msananga,
mradi huo awali ulikuwa utekelezwe katika wilaya ya Ulanga na Kilombero,
lakini baada ya Ulanga kugawanywa na kuzaliwa wilaya mpya ya Malinyi
nayo imewekwa kwenye mradi huo.
Alisema lengo la mradi huo ni kupima kila kipande cha ardhi kilichoko
katika wilaya hizo na kuwapa hati miliki za ardhi pamoja na hati miliki
za kimila kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini.
Mradi wa uwezeshaji wa kumiliki ardhi (LTSP) chimbuko lake ni
kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za kundi la G8 kuhusu
uwazi katika sekta ya ardhi. Mpango huo unafadhiliwa na nchi za
Uingerea, Denmark na Sweden.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment