Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwassa.
MKUU wa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Betty Mkwasa, amemwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, kuchukua hatua za
haraka kwa watumishi waliosababisha jengo la vyumba vitatu vya madarasa
katika Shule ya Sekondari Wami kushindwa kutumika.
Jengo hilo lilijengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 300 na
limebainika kujengwa kwa kiwango cha chini na limejengwa kwa ufadhili wa
fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf). Mkwasa alisema ukaguzi
ulipofanyika ulibaini limejengwa chini ya kiwango na wanafunzi kushindwa
kutumia kutokana na ubovu huo wa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Alitoa agizo hilo alipotembelea shule hiyo mwishoni mwa wiki kwa
ajili ya kukagua shughuli za kitaaluma, mpango wa kumaliza changamoto ya
madawati, vyumba vya madarasa na vyoo. Katika ziara hiyo alijionea
jengo hilo la vyumba vitatu vya madarasa likiwa halitumiki kutokana na
nyufa nyingi ukutani na sehemu ya paa kuezuliwa na upepo.
Mkwasa pia aliagiza apatiwe taarifa ndani ya siku tatu kuanzia Machi
10 mwaka huu, kwa nini jengo hilo limejengwa chini ya kiwango wakati
majengo mengine shuleni hapo yamejengwa kwa ubora.
Alishangaa kwa nini uongozi wa halmashauri haujachukua hatua kwa
waliohusika na jambo hilo kwa kusababisha uwepo wa upungufu wa vyumba
vya madarasa na kuwafanya idadi kubwa ya wanafunzi kurundikana
madarasani.
“Jengo hilo limejengwa chini ya kiwango na hatua hazijachukuliwa, na
haiwezekani kukarabatiwa wakati waliosababisha wapo na hawajachukuliwa
hatua hadi sasa” alihoji Mkwasa.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Lupyana Kissiya, alisema wakati akihamia
shule hiyo mwaka 2013, alilikuta jengo hilo la vyumba vitatu
limekamilika lakini bila kutumiwa na wanafunzi kutokana na kubainika
kuwa ni bovu baada ya ya ukaguzi kugundua limejengwa chini ya viwango.
Alisema ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Idara ya Elimu Sekondari
wilayani humo, ilibaini hayo na kueleza kuwa jengo hilo halifai kwa
matumizi ya wanafunzi kwa kuwa linahatarisha usalama wao.
Kissiya alisema Idara ya Elimu ya Sekondari ilipendekeza mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri afahamishwe kwa barua, ambapo alimtuma mhandisi
wa ujenzi kulifanyia ukaguzi na mhandisi alipendekeza likarabatiwe
lakini ukosefu wa fedha umefanya lisikarabatiwe hadi sasa
Chanzo Habari leo
0 comments:
Post a Comment