Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI ya Mkoa wa Morogoro imeanza kuchukua hatua mbalimbali za
kuboresha mazingira ya kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa huo ili kuwezesha kukidhi mahitaji ya sasa.
Hatua hiyo imeanza kuchukuliwa kwa kushirikiana na hospitali hiyo
kutafuta wadau wa kusaidia kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la
kuhifadhi maiti ikiwa ni kuweka majokofu mapya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Dk Rita Lyamuya
alisema hayo jana mjini Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu utendaji kazi zinazofanyika hospitalini hapo.
Shughuli hizo ni za utoaji wa huduma za tiba kwa wagonjwa wa nje na
wanaolazwa na namna ya mazingira ya kuhifadhi maiti za watu wanaokufa
kwa ajali, vifo vya kawaida ama maiti zinazookotwa na kuletwa na Polisi
hospitalini kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Dk Lyamuya alisema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ndiyo pekee
inayotegemewa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya
Wilaya ya Morogoro kutokana na kutokuwepo kwa hospitali za wilaya.
Alisema kushamiri kwa matukio ya ajali za barabarani, majeruhi na
watu wanaopoteza maisha, miili yao inaletwa hospitali ya rufaa ya mkoa
na kuhifadhiwa chumba za maiti kilichopo katika hospitali ya rufaa ya
mkoa.
Alisema chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa hiyo
kina majokofu manne yenye uwezo wa kuhifadhi maiti 30, lakini hadi sasa
ni jokofu moja lenye uwezo wa kuhifadhi maiti sita ndilo linalifanya
kazi.
Pamoja na hayo, alisema majokofu mengine mawili katika chumba hicho
ambalo kila moja lina uwezo wa kuhifadhi maiti sita yanafanyiwa
matengenezo kutokana na hitilafu iliyokuwa imejitokeza.
“Kukamilika kwa matengenezo ya majokofu haya kutawezesha hospitali ya
rufaa ya mkoa ambayo ndiyo tegemeo kubwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi
maiti 18,” alisema Dk Lyamuya na kuongeza kuwa jokofu moja lenye uwezo
wa kuhifadhi maiti 12 halifanyi kazi kutokana na ubovu, hivyo kuhitajika
kununuliwa jingine ama kufanyiwa matengenezo makubwa sambamba na
maboresho ya mfumo mzima ya jengo hilo.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment