Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya watu 40 wanahofiwa kufa maji katika Mto
Kilombero baada ya kivuko walichokuwa wamepanda kuzama maji juzi saa
mbili usiku.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa wahanga wa
ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Shahib Msinduka,
alisema kivuko hicho kilizama baada ya kuzidiwa nguvu na maji
yaliyokuwa yakitoka upande wa kushoto kwao na hivyo kukizidi nguvu.
Hata hivyo mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Yahaya Masele ambaye
alikuwa upande wa pili wa Wilaya ya
Kilombero akisubiri kivuko hicho, alidai kuwa kilikuwa na
watu takribani 50 au 60 pamoja na magari matatu.
“Kwenye kivuko hicho kulikuwa na gari tatu ambazo ni Isuzu
Fuso lililobeba mpunga ,Toyota Land Cruiser pick up mali ya Kampuni ya
Mitiki na Land Cruiser Station Wagon mali ya Benki ya CRDB ambazo zote
zimezama katika mto huo,“ alisema shuhuda huyo.
Mashuhuda wengine walidai kuwa watu 15 waliokolewa na wengine sita walijiokoa wenyewe.
Walisema kuwa idadi kamili ya watu waliokuwamo kwenye kivuko hicho
bado haijajulikana rasmi licha ya watu wengine kudai kuwa walikuwa
zaidi ya watu 50.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Reff Gembe, alisema hadi sasa ni watu
watatu waliofariki dunia ambao ni wale waliokuwa kwenye magari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliothibitika kufariki dunia hadi sasa
ni Meneja mikopo wa benki ya CRDB Tawi la Kilombero pamoja na
vijana wawili waliokuwa kwenye Fuso ambao ndugu zao walifika na
kuulizia kukosekana kwao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na kampuni ya Wachina wanaojenga
daraja katika mto huo, wanajaribu kutafuta njia ya kuyaopoa magari hayo
matatu yaliyozama ili kuona kama kutakuwa na miili ya watu wengine.
“Kwa mujibu wa wafanyakazi, nimeambiwa kuwa kivuko hicho kilikuwa
na watu kama 30 -35, lakini mpaka sasa kwa mujibu wa taarifa tumeambiwa
kuna tofauti ya watu watatu ambao hawajaonekana,“
alisema mkuu huyo wa wilaya.
Aidha mkuu huyo alisema kuwa anaomba wananchi
kuwa watulivu wakati juhudi mbalimbali zinafanyika kutoa
magari yaliyozama ili kupata jibu sahihi la idadi ya watu waliopoteza
maisha katika ajali hiyo.
Tukio hilo la kuzama kwa kivuko hicho ni la pili katika mto huo
ambapo mwaka 2002 kilizama na kusababisha watu zaidi ya 30 kupoteza
maisha.
Aidha licha ya taarifa hiyo ya mkuu wa wilaya, kuna taarifa
ambazo hazikuthibitishwa zinazodai kuwa waliofariki kutokana na ajali
hiyo ya kivuko inaweza kufikia 40. kwani kwa kawaida kivuko
hicho huvusha wastani wa watu 50
hadi 60 kwa safari moja.
hadi 60 kwa safari moja.
CHANZO ; MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment