Na Mwandishi Wetu
UJANGILI uliokithiri nchini Tanzania
unatishia kudhoofisha uchumi wa nchi ambao unazidi kukua kutokana na sekta ya
utalii kuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa na katika kuongeza ajira.
Dk. Adelhelm Meru, Katibu Mkuu wa
Wizara ya maliasili na utalii, ameonya kwamba kuna uwezekano ujangili ukaathiri
ajira zipatazo milioni 3.8 kwenye sekta ya utalii katika ukanda wa Afrika
Mashariki wakiwemo waongoza watalii, madereva, mahoteli pamoja na wahudumu wa
migahawa.
Kwa mujibu wa shirika la All Africa
Tanzania pamoja na nchi nyingine barani Afrika zimeathirika sana kutokana na
ujangili katika miaka kumi iliyopita. Mwaka jana utafiti ulionyesha kuwa
Tanzania imepoteza zaidi ya nusu ya tembo wake ambapo idadi imepungua kutoka
tembo 110,000 mwaka 2009 kufikia chini ya tembo 44,000. Twiga pia ambao ni
alama ya taifa nao wamepungua kwa kiasi kikubwa.
Meru amesema kuwa japo majangili
wanazidi kunufaika na biashara hii, sekta ya utalii inaendelea kuumia. Amesema
Tanzania ina ajira 700,000 kutokana na utalii na anasema idadi hiyo ya ajira
inaweza kuongezeka mara mbili endapo ujangili uliokithiri kwa wanyamapori
utaisha.
Katika kuisaidia serikali ya
Tanzania hivikaribuni, mashirika ya Wildaid na African Wildlife Foundation
yalizindua kampeni mpya ijulikanayo kama “Ujangili Unatuumiza Sote” kwa
kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii. Kampeni hii inatumia viongozi wa
dini na watu maarufu katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu janga la ujangili
na pia kuwakumbusha Watanzania kulinda wanyamapori ambao ni fahari na rasilimali
kubwa kwa taifa.
Kampeni hii itatumia runinga, redio,
mitandao ya jamii, magazeti, vijarida, matangazo na filamu zitakazoonyeshwa
kwenye maeneo ya wazi ili kuwafikia wananchi waishio mijini na vijijini.
Utafiti uliofanywa na WildAid kwa
kushirikiana na African Wildlife Foundation kwa Watanzania kwa kuwahoji
Watanzania zaidi ya 2,000 waishio mijini na vijijini uligundua kwamba asilimia
80 kati yao wanaelewa madhara yanayoweza kuikumba Tanzania endapo tembo
watatoweka. Kati ya walihojika katika utafiti huo, asilimia 73 walisema kwamba
wanyama pori ni mojawapo ya alama za taifa na urithi wa taifa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu
wa Wildaid, Peter Knights amesema kwamba "Ujangili kwa tembo ni wizi
unaowaumiza Watanzania wa sasa na wa vizazi vijavyo. Tunaviomba vyombo vya
habari kushiriki katika kampeni hii na tunahitaji kila mmoja asaidie katika
mapambano kukomesha ujangili”.
Chanzo Mtaa kwa Mtaa Blog
Chanzo Mtaa kwa Mtaa Blog