Home » » Morogoro yaanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura

Morogoro yaanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. John Henjewele akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyofanyika Juni 5, 2015 Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. Kulia, ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Bi Azimina Mbilinyi.
Baadhi ya wajumbe wa mafunzo hayo wakila kiapo cha uaminifu katika utekelezaji wa zoezi ambalo liko mbele yao. Kushoto ni Hakimu Mkazi Bi. Agnes Ringo.
Bi. Sajira Mbaga ambaye ni Afisa kutoka tume ya Taifa ya Uchaguzi, akihojiwa nawaandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Baadhi ya vifaa vilivyowasili Mkoani Morogoro kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Picha na Andrew Chimesela 

Na Andrew Chimisela

Mkoa wa Morogoro umeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu.

Maandalizi hayo yameanza jana kwa semina ya siku mbili inayotolewa kwa waratibu wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika ngazi ya Mkoa na Wilaya za Mkoa wa Morogoro.
Semina hiyo inalenga kutoa Elimu itakayowawezesha kutekeleza jukumu hilo katika kufanikisha zoezi hilo muhimu. Mafunzo hayo yatahusisha ujazaji wa fomu zitakazotumika kwenye zoezi zima la uboreshaji la wapiga kura. 

Aidha, yatatolewa mafunzo kwa vitendo yatakayohusu jinsi ya kutumia kifaa cha kisasa yaani Biometric Voters Registration (BVR) kinachochukua alama mbalimbali za mpiga kura kwa lengo la kuondoa uwezekano wa mtu kujiandikisha zaidi ya mara mbili.

Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro  Dkt. Rajabu Rutengwe kupitia hotuba iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa  Mhe. John Henjewele,  aliwataka wanasemina kujifunza kwa bidii na kuhakikisha wanajua utaratibu unaotakiwa kutumika katika kuboresha daftari hilo la kudumu la wapiga kura.

Dkt. Rutengwe alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujiandikisha katika vituo vyao mara muda utakapowadia wa kufanya hivyo. “Naomba kutoa wito kwa wananchi walio na sifa ya kuwa wapiga kura Mkoani hapa waweze kujitokeza ili wajiandikishe”. Alisema.
“Aidha, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali Mkoani hapa imedhamiria kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa” Dkt. Rutengwe aliongeza.

Naye Bi. Sajira Mbaga, Afisa kutoka Tume ya Uchaguzi alisema, zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mkoa wa Morogoro, linatarajiwa kuanza kufanyika Juni 14 mwaka huu na kuongeza kuwa Tume hiyo inaendelea na jitihada za kuondoa changamoto zilizojitokeza kwenye zoezi hili katika Mikoa mingine ambapo zoezi hili limekwisha fanyika.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa