Home » » SEMINA YA USAMBAZAJI WA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012 YAFANYIKA MKOANI MOROGORO

SEMINA YA USAMBAZAJI WA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012 YAFANYIKA MKOANI MOROGORO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Na Veronica Kazimoto
Morogoro
4 Mei, 2015.
 
Usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni muhimu ili kila ngazi ya utawala iweze kuzipata, kuzielewa na kuzitumia takwimu zitokanazo na Sensa hiyo kwa ajili ya kutunga sera, kuandaa na kutathimini utekelezaji wa mipango ya maendeleo pamoja na kufanya maamuzi sahihi.
 
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe wakati akifungua Semina ya siku moja ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliyofanyika mjini Morogoro.
 
"Ni matumaini yangu kwamba, ninyi nyote mliokusanyika hapa  mtazitumia vizuri takwimu hizi ili ziwasaidie katika kuweka vipaumbele vya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mkoa wa Morogoro", amesema Dkt. Rutengwe.
 
Mkuu huyo wa Mkoa amesisistiza kuwa ni wajibu wa kila Ofisa wa Serikali mkoani Morogoro kuhakikisha takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinakuwa msingi wa mipango  ya maendeleo na kuwa kigezo cha kufanya maamuzi katika kuweka mstakabali wa mkoa wa Morogoro.
Nae  Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akitoa maelezo mafupi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, amesema lengo la Semina hiyo ni kuwaelimisha wadau katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri juu ya matumizi ya takwimu za Sensa ya Watu ili waweze kuzitumia katika kupanga na kutathmini program mbalimbali za maendeleo katika ngazi husika.
 
"Dumuni lingine la Semina hii ni kuhamasisha matumizi ya takwimu rasmi katika shughuli zetu za kikazi, ili lengo la kutumia takwimu za Sensa kuboresha maisha ya Mtanzania liweze kutimia", amesema Kwesigabo.
 
Kwesigabo amefafanua kua Semina hiyo ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi itasaidia kujua ni maeneo yapi mkoa wa Morogoro umepiga hatua na maeneo ambayo yanapaswa kutiliwa mkazo ili kuweza kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa.
 
Jumla ya washiriki mia moja na kumi (110) kutoka ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote mkoani Morogoro wameshiriki katika Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa lengo la kupata elimu juu ya matumizi ya takwimu zinazotokana na Sensa hiyo.
 

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa