Home » » WAGOMA KUPISHA MRADI WA BWAWA

WAGOMA KUPISHA MRADI WA BWAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKAZI wa vijiji vya Bwirachini na Kiburungo Kata ya Selembala Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini wamegoma kuondoka kwenye makazi yao kupisha mradi wa bwawa la kufua umeme la Kidunda hadi tathmini ya malipo itakapofanyika upya.
Wanakijiji hao wamefikia hatua hiyo huku uongozi wa Wilaya ya Morogoro kupitia kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo mwaka 2011, Said Mwambungu na Mbunge Innocent Kalogeresi kuwakutanisha na kuweleza mpango wa mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kwa kuruhusu mradi  huo wa bwawa la kufua umeme la Kidunda uwekezwe  kijijini humo.
Wanakijiji hao, walielezwa manufaa mbalimbali watakayopata kupitia mradi huo kuwa ni kujengewa barabara itakayounganisha vijiji vya Bwirachini na Kiburungo na pia watatumia maji ya bwawa hilo kwa kilimo cha umwagiliaji.
Wakiwa katika mkutano maalumu uliowakutanisha zaidi ya wananchi 2,000 wa vijiji hivyo, walitishia kuandamana hadi Ikulu kufikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete, ili awasaidie warudishiwe maeneo yao waliositishwa kuyaendeleza kwa ajili ya kupisha mradi huo.
Katika mkutano huo uliyokuwa na lengo la kutoa azimio juu ya uwekezaji mradi huo, baadhi ya wanakijiji Iddi Mkanga, Sofia Makimila, Sharifa Rajabu, Msafiri Gila na Kibwa Salehe, walisema utekelezaji mradi huo umeanza kuonyesha dosari mapema kutokana na fidia walizopangiwa kulipwa kutozingatia uhalisia wa mali.
Dosari nyingine zilizoanishwa na wananchi hao ni pamoja na vipimo vya ukubwa wa bwawa hilo, kutowasilishwa kijijini hadi sasa na eneo la viwanja walivyopangiwa kuhamia si chaguo lao, hali ambayo inawajengea hofu kuwa mradi huo utaongeza ugumu wa maisha badala ya kuleta maendeleo.
Ili waweze kupisha utekelezaji wa mradi huo, walitaka matengenezo ya barabara inayounganisha vijiji vya Bwirachini na Kiburungo, eneo watakalohamia wachague wao wenyewe na bwawa hilo liwe katikati ya vijiji hivyo ili upande wa pili yawe mashamba ya umwagiliaji.
Awali, Katibu wa Kamati ya ufuatiliaji mradi huo kwa wakazi wa Dar es Salaam, Yahya Mkanga na Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwirachini, Mohamed Kinyogoli, walisema wana wasiwasi wanaweza kudhulumiwa haki zao kupitia mradi huo, kwa sababu hadi sasa haijulikani vipimo halisi vya ukubwa wa eneo linalohitajika kwa mradi huo.
Hofu nyingine iliyojengeka kwa viongozi hao, ni hatma ya fidia yao ambayo bado haijawekwa wazi na halmashauri, ndiyo maana wameazimia kutoondoka hadi makubaliano yafanyike upya.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa