Home » » RC: WANANCHI MSIPUUZE TAARIFA ZA HALI YA HEWA

RC: WANANCHI MSIPUUZE TAARIFA ZA HALI YA HEWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATENDAJI wa idara mbalimbali na wananchi wametakiwa kutopuuza taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), kupunguza madhara yanayotokea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Aidha, TMA imetakiwa kutoa utabiri kwa lugha nyepesi na wakati sahihi ili kufikisha taarifa kwa umma zilizo sahihi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alisema hayo jana wakati wa kufungua warsha ya waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, ushirikishwaji na usambazaji wa taarifa hizo kwa umma.
Bendera alisema lazima wananchi wapate na kufanyia kazi taarifa za mamlaka hiyo kujiepusha na majanga.
Alisema kumekuwa na kawaida kwa TMA kupeleka taarifa hizo kwa wakuu wa mikoa na wakuu hao kutoa taarifa hizo kwa wakurugenzi na wakuu wa wilaya, lakini wapo wanaopuuza bila kupanga mikakati ya kukabiliana na madhara, yatakayotokea kutokana na utabiri huo.
“Kuna watu wakisikia taarifa hizo wanapuuza na kubeza kiasi ambacho hata wakiambiwa watoke maeneo hatarishi hawakubali, ni lazima watendaji kuwa wakali kufanyia kazi taarifa hizi kwa kupanga maeneo ya kuwapeleka pale mnapotaka waondoke maeneo yenye mafuriko au ukame,” alisema.
Alitaka TMA kujitafakari juu ya sababu ya taarifa zao kutofanyiwa kazi ipasavyo.
“Kuna maneno ya kitaalamu wanayotumia wanasayansi wa hali ya hewa, ni muhimu yakatafsiriwa kwa lugha rahisi ili wananchi waelewe na kutumia taarifa hizo kwa usahihi, lakini wapo watu wabishi kuhama mabondeni licha ya kupewa taarifa hizo na ndiyo tunaokwenda kuwaokoa baada ya mafuriko,” alisema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema mamlaka hiyo hutoa taarifa kila mara, kuhakikisha Watanzania hawapati athari zitokanazo na hali ya hewa.
Alisisitiza ushirikiano wa ofisi yake na waandishi wa habari ni muhimu katika kufikisha taarifa sahihi kwa jamii. Pamoja na warsha hiyo, Dk Kijazi alisema wataalamu wa mamlaka hiyo watatoa taarifa za utabiri kwa msimu utakaoanza Oktoba hadi Desemba.
Alisema ni mara ya kwanza kwao kutoa utabiri wa msimu nje ya Dar es Salaam.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa