Home » » CWT YAWAZAWADIA WALIMU WASTAAFU

CWT YAWAZAWADIA WALIMU WASTAAFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
CHAMA cha Walimu (CWT) manispaa ya Morogoro kimeanzisha utaratibu mpya wa kuwazawadia walimu wake wastaafu samani mbalimbali kama shukrani ya utendaji wao wa kazi kwa miaka waliotumikia.
Akikabidhi zawadi ya mifuko ya saruji 130 kwa walimu 13 wa shule za msingi, sekondari na waratibu elimu wa kata waliostaafu, Rais wa chama hicho taifa, Gratian Mkoba alisema, kuwa walimu ni hazina kubwa katika jamii hivyo wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
Raisi huyo aliwataka walimu hao wastaafu kuendelea kuungana na chama hicho kupinga sheria kandamizi zinazoingizwa kwenye mifuko ya taifa ya hifadhi ya jamii, ikiwemo zile zinazolenga kuwapunja wastaafu mafao yao.
Mkoba alipongeza tawi hilo la Morogoro kutokana na ubunifu walioanzisha wa kuwazawadia walimu hao kwani utaratibu huo haujawahi kufanywa popote.
 “Pamoja na walimu kutumikia taaluma ya ualimu ambayo ni kitovu cha taaluma zingine, bado watawala wa nchi wameendelea kutoithamini taaluma hii kama inavyostahili,” alisema
Aidha wastaafu hao waliiomba CWT kuwaruhusu  kuendelea kuwa wanachama wa chama hicho ili wapate kupaza sauti zao na kuzungumzia kero zinazowakabili hasa ya kuhusu mafao yao.
Akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, Anna Mapunda alisema kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao na hata kuchukua muda mrefu ikiwemo  malipo ya kusafirishia  mizigo yao.
Naye Katibu wa chama hicho mkoani humo, Mnada Maswi, alisema msaada huo umetokana na bajeti waliyotenga tangu mwaka 2013 ili kuwapa zawadi walimu wanaostaafu ambao walishiriki kikamilifu kukiimarisha chama hicho kwa uaminifu.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa