Home » » MOROGORO WATAKA VIGOGO WANYANG'ANYWE ARDHI

MOROGORO WATAKA VIGOGO WANYANG'ANYWE ARDHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
DIWANI wa Mafisa, Manispaa ya Morogoro, Francis Kayenzi, amelaumiwa kutokana na hatua ya vigogo serikalini kuchukua viwanja na kuvitelekeza katika kata yake.
Wananchi wa kata hiyo, wamemtaka diwani huyo kuhakikisha viwanja hivyo vilivyotelekezwa vinachukuliwa na serikali na kugawiwa wanyonge.
Walibainisha kuwa kutelekezwa kwa viwanja hivyo kunatokana na vigogo waliopewa kutokuwa na msukumo wa kujenga na badala yake vimegeuka mapango ya wabakaji, wezi, wadudu na wanyama wakali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya diwani huyo, baadhi ya wananchi akiwemo Godwin Mjema na Steven Kiswaga, walisema kata hiyo ambayo sasa ipo katikati ya mji, viwanja vyake vimetelekezwa na waliopewa kwa tamaa huku wengine wakivigeuza mashamba ya misitu.
“Tunasema mwandikie barua maalumu rais afute hati hizi ili viwanja hivi vigawiwe kwa mara nyingine walalahoi… viwanja hivi ni vya wakubwa serikalini, ambao hawana shida na ardhi, wamevichukua kwa tamaa ili waje watuuzie kwa bei ya kuruka,” alisema Mjema.
Katika ufafanuzi wao, walimtaja aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mathew Sedoyeka kuwa miongoni mwa vigogo waliochukua maeneo katika kata hiyo, kisha badala ya kujenga amepanda miti na kugeuka msitu ambao ni pango la wezi.
Akijibu madai hayo, mbali na kuahidi kufuatilia hatima ya viwanja vilivyotelekezwa katika kata hiyo, Diwani Kayenzi aliwaagiza viongozi wa mitaa kujadili kwenye vikao vya wananchi na kuandaa mapendekezo yatakayomwezesha kuchukua hatua za kisheria.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa