Home » » TEMBO WAWILI WAUAWA,WANG'OLEWA MENO

TEMBO WAWILI WAUAWA,WANG'OLEWA MENO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo
 
Wakati serikali ikisitisha Operesheni Tokomeza iliyokuwa ikifanyika pembezoni mwa hifadhi mbalimbali nchini ili kudhibiti vitendo vya ujangili, vitendo hivyo vimeanza tena, baada ya tembo wawili kuuawa kwa risasi na kung’olewa meno manne ndani ya hifadhi ya Taifa Udzungwa, iliyopo Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na wananchi wanaopinga vitendo hivyo walifanikiwa kumpata mmoja wa watuhumiwa wa ujangili huo ndani ya hifadhi hiyo.

Akizungumzia tukio hilo kwa waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema majangili hayo baada ya kusikia milio ya risasi wananchi walikusanyika na kuanza kufuatilia kwenye hifadhi hiyo.

Kamanda Paulo alisema wakati wananchi wakifuatilia, majangili hayo yalipata hofu na kutoweka.

Hata hivyo, wananchi walifanikiwa kuwakuta tembo wawili madume wakiwa wameuawa, huku wakiwa hawana meno.

Alisema baada ya kuendelea kufuatilia, waligundua meno hayo kufichwa kwenye msitu wenye majani na yalikuwa bado mabichi na yenye damu.

Kamanda Paulo alisema juhudi za wananchi kwa kushirikiana na polisi Julai 26, majira ya saa 11:30, walifanikiwa kukamatwa kwa mtuhumiwa, Fidelis Mohamed.

Alisema katika kumhoji, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na ujangili huo na alionyesha silaha iliyotumika kuua tembo hao, ambayo ni Rifle 375 yenye namba TZ 43818 NP 19 pamoja na shoka lililotumika kung’olea meno ya tembo hao baada ya kuwaua.

Kamanda Paulo alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na jitihada za kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo, ambao mtuhumiwa huyo aliwataja zinaendelea.

 Aliwapongeza wananchi kwa kuitikia wito wa operesheni hiyo shirikishi pia aliwaomba wananchi wengine kuiga mfano wa wananchi wa kitongoji cha Kidiya, ambao wanaendelea kushirikiana na polisi katika kufichua uhalifu.

Wakati huo huo, Kamanda huyo wa Mkoa wa Morogoro, alisema polisi imejipanga vyema kwa kuendesha doria wakati wote wa kusherekea sikukuu ya Iddi na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wote wanapokuwa kwenye nyumba za ibada na kumbi za starehe.

Pia amewataka wananchi kutoondoka majumbani pasipo kuchukua tahadhari na kutoa ushirikiano kwa polisi kufichua vitendo vya kihalifu na viashiria vyake ili kuwezesha wananchi kusherehekea sikukuu kwa amani na utulivu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa