Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia bingwa wa ngumi za
kulipwa duniani, Francis Cheka ‘SMG’ kwa tuhuma za kumchapa Meneja wa
baa ya Vijana Social Hall iliyopo Kata ya Sabasaba, Manispaa ya
Morogoro.
Kwa mujibu wa maelezo ya meneja huyo, Bahati Kabanda ‘Masika’ (39),
Cheka alifika katika baa hiyo majira ya jioni na kuanza kumtukana na
kumshambulia kwa maneno machafu kisha kumvamia na kuanza kumchapa ngumi
na mateke sehemu za tumboni.
Kwamba ni tukio la Juni 2, mwaka huu katika baa hiyo inayomilikiwa na promota wa ngumi za kulipwa mkoani hapa, Zumo Makame.
Kabanda amedai wakati akipewa kichapo na Cheka, hakuna mtu aliyesogea
kuamulia ugomvi huo kutokana na watu kumuogopa bondia huyo aliyewahi
kuwapiga mabondia wa ndani na nje ya nchi.
Alidai Cheka alifika katika baa hiyo na dalili za kulewa pombe na
baada ya kuondoka, wasamaria wema walimchukua yeye hadi katika
hospitali ya rufaa ambako alilazwa na kupatiwa vipimo na matibabu ya
maumivu aliyoyapata.
Kabanda alidai kuwa hakuwa na ugomvi na bondia huyo, na hivyo hajui
chanzo cha kupigwa na kuongeza kuwa kama alikuwa na ugomvi nae
angemfikisha kwenye vyombo vya sheria na sio kujichukulia sheria
mkononi.
Masika alidai kuwa pamoja na kupatiwa matibabu, lakini bado hali yake
kiafya sio nzuri kutokana na maumivu aliyoyapata ya mbavu, hivyo
kumfanya ashindwe kutembea vizuri.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa walimuona Cheka
akimuangushia kipigo meneja huyo, lakini walishindwa kuamulia ugomvi
huo kutokana na kumwogopa Cheka ambaye ni bingwa wa ngumi duniani.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Ritha
Lyamuya, alikiri kumpokea Masika hospitalini hapo Juni 2, akiwa na
maumivu ya mbavu na walipompima X-ray ilionekana amepata maumivu, hivyo
walimpatia matibabu na kumruhusu kurudi nyumbani.
Alisema hadi anaruhusiwa hospitalini hapo, Masika alikuwa anaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, amekiri Cheka kufanya
shambulio hilo kwa meneja huyo kwa kumpiga sehemu za tumboni na
kichwani.
Paulo alisema Cheka amekamatwa na anashikiliwa na polisi kwa
mahojiano na kwamba katika maelezo yake, anadai kuwa yeye na Masika
walikodi baa hiyo na kufanya biashara kwa pamoja, lakini baadaye
walianza kukosana katika suala na mapato.
Cheka aliendelea kudai kuwa siku ya tukio alifika katika baa hiyo kwa
lengo la kutaka kujua namna mauzo yanavyokwenda, lakini meneja huyo
alimzuia kuingia kaunta na ndipo ilitokea kutoelewana na baadae ugomvi
huo kutokea.
Kamanda Paulo alisema pamoja na maelezo hayo ya Cheka, lakini
ameiagiza timu ya askari kuchunguza kwa kina tukio hilo ili sheria
iweze kuchukua mkondo wake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment