Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATOTO wanaoishi katika mazingira magumu katika Manispaa ya
Morogoro, wameandamana mjini hapa wakishinikiza kupatiwa ulinzi wa
kutosha.
Watoto hao walitoa ombi hilo juzi, baada ya maandamano ya kuadhimisha Siku ya Haki ya Mtoto.
Walisema wanashangazwa na usimamizi wa sheria zilizopo licha ya nchi
kutunga na kuridhia mikataba mingi ya kimataifa yenye mwelekeo wa
kuwalinda.
Mmoja wa watoto hao, Veronica Omari, alisema wamechoshwa na taarifa
mbaya dhidi yao zisizotafutiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwemo kuwakamata na
kuwahukumu watu wanaoendeleza vitendo viovu, jambo ambalo
linawasababishia unyonge.
“Watoto tunauawa, tumekuwa chombo cha kukidhi haja za kimwili kwa
watu wazima wakiwemo ndugu zetu, ushirikina na yote haya yanafanyika
kwa kuwa hatuna wa kututetea kwa kuwa serikali haitujali… tunaomba
serikali itutengenezee mazingira bora ya usalama na hadhi zetu,”
alisema Veronica.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
mwakilishi wake, Clemence Matata kutoka dawati la kupinga unyanyasaji
wa kijinsia na ukatili kwa watoto, aliwataka watoto kufunguka kwa kutoa
taarifa kwa jeshi hilo na watakuwa tayari kuwalinda na kuwatetea.
Awali waratibu wa hafla hiyo akiwemo Mratibu Mkuu wa Ustawi wa Jamii,
Amani Center, Elly Maarifa na Mkurugenzi Mtendaji wa World Vision
Tanzania, Rehema Mwbwala kwa niaba ya asasi ya kimataifa ya Save Family
Tanzania Charity (SFTC), waliiomba serikali kuzitekeleza sheria na
mikataba ya watoto ambayo Tanzania imeridhia.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment