Home » » MWEKEZAJI ALIYEPOKWA ARDHI KUDAI FIDIA

MWEKEZAJI ALIYEPOKWA ARDHI KUDAI FIDIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
BAADA ya Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kuligawa eneo la mwekezaji Mees Estate Ltd kwa wanakijiji cha Mbigili, Kitongoji cha Mateteni kwa madai kuwa imefutiwa umiliki, uongozi wa mwekezaji huyo umeibuka na kulaani kitendo hicho na kudai fidia ya zaidi ya sh milioni 800.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, mmoja wa wakurugenzi wa Mees Estate Ltd inayomiliki mashamba ploti namba 28, 29 na 32, Patrick Mees, alisema chokochoko dhidi ya mashamba hayo yenye ukubwa wa ekari 1,466 zimesababisha kushusha uzalishaji mwaka huu na kuamsha hofu dhidi ya uhai wao na mali shambani hapo.
“Mashamba haya tunayamiki kihalali kwa hati ya umiliki ya 1987 na tangu kipindi hicho tunayatumia kuzalisha zaidi ya tani 25,000 za aina mbalimbali za nafaka ukiwemo Mpunga na Mahindi, licha ya uwekezaji mwingine kama majengo, mifugo, majosho na msitu wa miti ya mbao aina ya Mkongo,” alisema.
lisema Mees Estate Ltd inaheshimu mamlaka ya nchi, licha ya serikali kupuuza hata zuio la mahakama la Desemmba 30, mwaka 2010 na kazio la Agosti 6, mwaka jana dhidi ya kesi ya msingi namba 314/2010 katika Mahakama Kuu ya Ardhi, Kanda ya Dar es salaam.
“Tumekuwa wavumilivu kwa muda mrefu sana, lakini sasa hasara hii mwaka huu hatutaivumilia tutakwenda kudai fidia ya zaidi ya milioni 800 ya thamani ya ardhi, vitu vilivyowekezwa na usumbufu ambao sasa tunaupata kutokana na mashinikizo ya serikali katika ardhi yetu,” aliongeza Patrick.
Juzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi wilayani humo, Anna Sanga, Ofisa Ardhi Wilaya, Arnold Selestine na Mwanasheria wa Wilaya, Ocate Maganiko walifika katika kitongoji cha Mateteni na kuuagiza uongozi wa kijiji hicho kugawana mashamba ploti namba 28,29 na 32.
Kwa mujibu wa viongozi hao kijijini hapo,uamuzi wa halmashauri hiyo kugawa shamba hilo unatokana mashamba hayo kufutiwa umiliki wake na rais mwaka 2000 kisha kurejeshwa kwa wananchi.
Kuhusu kesi kuhusiana na mashamba hayo, Mwanasheria Maganiko alisema kesi zinazotajwa kuwepo Mahakama Kuu zilishafutwa na Mees EstateLtd yupo kimakosa katika eneo hilo.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa