Home » » KILOSA INA UPUNGUFU WA WALIMU 90

KILOSA INA UPUNGUFU WA WALIMU 90

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wanafunzi wakiwa darasani.
 
Wilaya  ya Kilosa Mkoani Morogoro inakabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo kwa kiwango kikubwa yamechangia elimu kudorora.
Matatizo hayo ni pamoja na upungufu wa walimu zaidi ya 90 katika shule za msingi, walimu kutopandishwa madaraja, kisa bajeti ndogo, wastaafu hawajalipwa stahiki zao, na pia hakuna shule yenye nyumba za walimu au ofisi za walimu.

Hayo yalielezwa mwishoni  mwa wiki na Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Kilosa, Rashidi Chayeka.

Afisa Elimu alisema upungufu huo umejitokeza baada ya jumla ya walimu 120 kupangwa katika wilaya hiyo lakini walioripoti ni 108 tu.

Akasema kwa sasa  wilaya ina upungufu wa walimu wapya 70 na walimu 20 wanatakiwa kustaafu  mwishoni mwa mwezi ujao.

“Shule za wilaya ya Kilosa zina upungufu wa walimu zaidi ya 90. Shule zote za msingi zina walimu watatu na wakizidi ni wanne tu kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.”alisema Afisa huyo.

Alitaja matatizo mengine kuwa ni miundo mbinu mibovu kutokana na mafuriko ya mara kwa mara yanayochangia kubomoka kwa madarasa na hakuna shule ambayo ilishawahi kuwa na nyumba za walimu wala maabara, wala ofisi ya kudumu ya kufaa kutunza vitabu vya kiada vya kusomea.

“Tatizo la vitabu vya sasa ni idadi ya maswali kuwa na mapungufu… inatakiwa maswali 50 lakini unakuta yapo jumla ya maswali  matano hadi saba. Pia alisema mada hazifafanuliwi vya kutosha ikiwa ni pamoja na mapungufu ya kurasa”, alidai Afisa wa elimu.

Aliongeza kuwa kiwango cha ufaulu ni cha wastani kutokana na jamii ya wamasi kuhamahama kila wakati, hali inayochangia shule yao ya Parakayo iliyoko kata ya Kimanga kukosa wanafunzi wanaotakiwa kujaza darasa kwani wakifaulu kumi wanaoripoti ni wawili tu.

Kwa tatizo la wanafunzi kupata mimba, alisema limepungua kwani kuanzia mwaka 2012 waliopata mimba walikuwa wanafunzi 43 ikilinganishwa na  mwaka 2013 ambapo waliopata mimba walikuwa sita tu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa