Home » » ASKOFU TAG ATAJA SABABU ZA WATANZANIA KUTOPIGA KURA

ASKOFU TAG ATAJA SABABU ZA WATANZANIA KUTOPIGA KURA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imeshauriwa kuangalia upya siku za upigaji kura katika uchaguzi zake mbalimbali zinazowahusisha wananchi wote hususani zile za udiwani, ubunge na urais ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujitokeza.
Rai hiyo ilitolewa leo na Askofu Paul Meivukie wa kanisa la TAG mkoani Tabora, katika sherehe za maadhimisho ya miaka 75 ya kanisa hilo hapa nchini, zilizofanyika katika viwanja vya kanisa la Kitete Christian Center mjini hapa.
Askofu huyo alisema mwitikio wa upigaji kura katika uchaguzi zilizo nyingi hapa nchini umezidi kushuka; kutokana na wananchi wengi kutojitokeza kwa wingi, jambo ambalo alidai linachangiwa na upigaji kura kufanyika siku za ibada.
Alisema siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ni siku rasmi za ibada hivyo kuweka uchaguzi katika siku hizo inakuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi walio wengi kutojitokeza kwa wingi katika upigaji kura.
"Tunaomba upigaji kura usiwekwe siku ya Ijumaa au Jumapili kwa maana siku hizi zinajulikana wazi kuwa ni siku za ibada kwa makundi ya Wakristo na Waislamu," alisema.
Alibainisha kuwa uamuzi wa serikali wa kuendesha chaguzi za kitaifa siku za Jumapili unawakosesha wananchi wengi haki zao za msingi za kuchagua viongozi wanaowapenda, hivyo akaiomba Serikali kulitazama upya suala hilo.
Aidha alisema ni dhahiri siku ya kupiga kura ikibadilishwa takwimu za wapiga kura zitaongezeka kuliko ilivyo sasa, kwa sababu watu wengi wanaona ni bora wakamwabudu Mungu wao siku hiyo kuliko kwenda kupanga foleni ya kupiga kura.
Akizungumzia mchakato wa katiba mpya unaoendelea hivi sasa kule Dodoma, Askofu alisema kanisa la TAG linaendelea kuliombea taifa ili livuke kipindi hiki kwa amani na kwa ushindi mkubwa huku akiwataka wajumbe wa bunge hilo kuwa makini sana ili wasichafue jina na taswira nzuri ya Tanzania.
 Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa